Umeacha hadhiti nzuri ya kusimulia kwa vizazi vya leo

NA ANTHONY MTAKA

UMEHITIMISHA safari yako duniani ukiwa ni mwenye Hadithi nzuri ya kusimuliwa kwa vizazi vya leo na vijavyo kama ulivyotuasa katika moja ya hotuba zako "Maisha ya Mwanadamu ni Hadithi tu hapa ulimwenguni"

Katika mengi mimi nitasimulia maeneo machache matatu. Moja,Watanzania walio wengi wanakusimulia kama Moja ya Kiongozi uliyefanikiwa kuwa Baba na Mlezi mwema wa watoto na familia yako,hata sifa nyingi tunazosimuliwa kuhusu unyenyekevu, uungwana na Utu zinajitafsiri miongoni mwa watoto,wajukuu na vitukuu wako ambao baadhi tumebahatika kuwaona na kuwafikia.
Viongozi na Watanzania wa kizazi chako na cha sasa wanakusimulia na kukushuhudia kama Baba wa Mageuzi,mimi nasema Mzee Mwinyi ulijenga kizazi cha Dhahabu kwenye ( Sekta Binafsi na Uongozi) ya Tanzania-Wafanyabiashara na Matajiri wakubwa wa nchi yetu ambao wamedumu kwa miaka wastani 40 walijijenga na kuwa na msingi imara kwenye awamu yako.

Naamini Mzee Bakharesa,na Marehemu Mzee Mengi ni moja ya mifano michache katika wengi waliofaidika na mageuzi yako kiuchumi mapema baada ya kumrithi Mwana Mwema wa Taifa letu Baba wa Taifa Mwl Nyerere.

Kizazi cha Dhahabu kwenye uongozi wako ni Matunda ya Mawaziri wako 2(Hayati Benjamini Mkapa na Dr Jakaya Kikwete kuja kuwa Viongozi wakuu wa Nchi yetu,Waziri wako Mama Anna Makinda alikuja kuwa Spika wa kwanza Mwana Mama wa Bunge la nchi yetu) hata leo Chama chetu Cha Mapinduzi bado kinayafaidi matunda ya kizazi chako cha dhahabu katika uongozi ambapo Comrade Kinana ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Tz Bara.

Achilia mbali heshima kubwa waliyojijengea viongozi uliofanya nao kazi ambao wapo hai leo kwa uchache-Mzee Malicela,Mzee Jaji Warioba,Mzee Msuya,Mzee Mangula aliyewahi kuwa Mkuu wako wa mkoa.

Heshima na haiba wanayoibeba leo kwenye umma wa nchi yetu vina akisi malezi mazuri na bora kutoka Baba wa Taifa na wewe uliyewapokea ukaendelea kujenga nao nchi,bila kusahau uthubutu wako wa kuyabeba mageuzi ya vyama vingi na leo vyama husika vimekuwa na mchango katika ustawishaji wa demokrasia ya nchi yetu.

Dunia inamsimlia Nelson Mandela kama kielelezo cha Msamaha-Kwangu mimi naamini na kwa Watanzania waliosikiliza au kusoma uchambuzi wa kitabu chako-Wanakubaliana kwamba wewe ni Baba wa Msamaha.

"Uliondolewa kwenye nyumba kwa lugha yenye maneno magumu na waziri mwenzako,akakatalia matofali na bati ulizonunua kwa mshahara wako ili ujenge nyumba yako ya kuishi" ukaja kuwa Rais na bado UKAMTEUA mtu aliyekutendea hayo magumu kuwa Waziri wako"Yataka moyo wenye hofu ya Mungu" 

 Hata aliyetoa chumba chako akampa mtu mwingine wakati unakuja kwenye mkutano wa CCM Dodoma,ukalazimika kwenda kulala kwenye Double Deka za wanafunzi wa chuo cha CBE ukiwa na wajumbe wengine,naye ulimsamehe na ulipokuja kuwa Rais UKAMTEUA.

Wewe ni Baba wa Msamaha-Hadithi yako ina mafunzo makubwa sana kwa sisi viongozi wa leo na wajao,inayo mafunzo kwa vizazi vya sisi wanadamu tulioumbwa kwa mfano wa Mungu.

Nakushukuru sana kwa kunipokea tukafanya mazungumzo enzi nikiwa Dc Mvomero nawe ukiwa unakuja shambani kwako (2012-2014) Dakawa,nakushukuru kwa mazungumzo nikiwa Rc Dodoma na zaidi nilipopata nafasi ya kuongea nawe na kukudadisi mawili matatu nilipofika nyumbani kwako Zanzibar kuhani msiba wa Mwanao mwaka 2023.

Nimejifunza mengi katika kukutana kwetu Umetuachia Utajiri Mkubwa wa Kitabu Chako,hatutaishia kusimulia hadithi ya Maisha yako,tutafanya hata nukuu za Kitabu chako ili hadithi yako nzuri uliyotuachia iendelee kuvifaa vizazi vya leo na vijavyo.

Mungu akupe pumziko la milele Mbinguni Ewe Mwana Mwema wa Taifa Letu,Balozi halisi wa Lugha yetu ya Taifa Kiswahili, Mwana Mageuzi Halisi wa siasa na Uchumi wa nchi yetu.

Natoa pole nyingi sana Kwa Mheshimiwa Rais Dr Samia Suluhu Hassan kwa kuondokewa na moja nguzo kwenye msingi Imara(wa Mzee Mwenye Busara,hekima na Hata ushauri) Nawapa Pole wana Familiya wote wa Mzee Mwinyi-Kaka na Rafiki yangu Mh Rais wa ZNZ Dr Hussein Mwinyi,Kaka Dr.Dulla,Kaka Abbas,Kaka Makame,watoto,wajukuu,vitukuu.

Natoa Pole Nyingi sana Kwa Watanzania wenzangu Wote ambao tulizifaidi hotuba zake zilizokuwa zinabeba Kiswahili Fasaha.

Anthony Mtaka
Rc Njombe

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news