Usiyoyafahamu kuhusu miaka mitatu ya NHIF kupitia Serikali ya Awamu ya Sita

DAR ES SALAAM-"Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ni taasisi iliyoanzishwa kwa Sheria Sura Na. 395 na lengo lake kubwa ni kusimamia upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wote waliosajiliwa na mfuko.

“Na mfuko huu ni matokeo ya maboresho katika Sekta ya Afya. Sekta ya Afya imetoka mbali wote tunafahamu baada ya Uhuru huduma hizo zilikuwa zikitolewa kwa kugharamiwa na Serikali;
Hayo yamebainishwa leo Machi 7,2024 na Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Bernard Konga wakati akiwasilisha mada kuhusu mafanikio ya mfuko huo kwa kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Ni katika kikao kazi baina ya wahariri wa vyombo vya habari na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam.

“Serikali ilikuwa ikigharamia kwa asilimia 100,lakini tulipoingia miaka ya tisini tulipoingia kwenye mitikisiko ya kiuchumi, Serikali ikaamua kuanzisha dhana nzima ya uchangiaji.Fahamu kuhusu Kitita kipya cha NHIF>>> 

“Ilivyoanzisha uchangiaji watu pia, ikaonekana sasa ugonjwa unakuja bila taarifa, ugonjwa unakuja unakuta Mtanzania hana fedha anajikuta hawezi kupata utaratibu wa matibabu.

“Kwa hiyo hapo, Serikali iliamua kuanzisha sasa utaratibu wa malipo kabla ya huduma, kwa hiyo iliruhusu kwanza makampuni binafsi kuingia sokoni. Lakini, pili ikafanya pilot kuwa na prepayment schemes za Serikali.

"Na mwaka 1996 wakapitisha sheria ya kuanzisha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa sekta rasmi hususani kwa watumishi wa umma,lakini pia wakaanzisha Mfuko wa Afya ya Jamii kwa ajili ya sekta isiyo rasmi.

"Ndiyo maana tukasema ni sehemu ya maboresho, katika sekta ya afya ambayo iligusa kwenye prepayments schemes na ndiyo NHIF ikaja tangu kuanza kwa utekelezaji wa majukumu yake tumeona kuanzia ugaharamia wa matibabu nchini, imekuwa ni mkombozi kwa wale ambao wamejiunga na imekuwa ni mfano.”

Amesema, mafanikio hayo ya zaidi ya miaka 23 ndiyo yaliipa Serikali msukumo wa kuona kuna umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya ya Matibabu kwa Wote nchini ambapo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeendelea kuboresha huduma kwa wanachama nchini.

Lengo likiwa ni kuhakikisha wanachama wa mfuko huo wanapata huduma bora na stahiki kwa maendeleo ya ustawi wa afya zao.
Konga amesema, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita,mfuko umeendelea kusajili wanachama wachangiaji, idadi ya vituo pamoja na kukusanya michango katika utoaji huduma.

Konga amesema, hadi kufikia Desemba 2023, NHIF una jumla ya vituo 9,467 vilivyosajiliwa ili kutoa huduma kwa wanachama wake.

Amesema, kati ya vituo hivyo 6,852 sawa na asilimia 72 ni vya Serikali huku vituo binafsi vikiwa ni 1,766 sawa na asilimia 19 ambapo kwa upande wa vituo vya madhehebu ya dini ni 849 sawa na asilimia tisa.

Konga amesema, wamefanikiwa kuongeza wanachama katika mfuko huo kwani ulipoanzishwa mwaka 2001/2002 walikua na wanachama 164,708 huku wanufaika wakiwa laki 691,773.

Mkurugenzi Mkuu amesema,mpaka kufikia 2023/2024 wameongezeka wanachama na kufikia 1,246,046 huku wanufaikia wakifikia milioni 4,987,292 ambalo ni ongezeko kubwa kwa muda mfupi.

Elimu kwa umma

Amesema,pia wanaendelea kutekeleza mpango wa uhamasishaji wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kupima afya ili kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Konga amesema, wamekuwa wakitumia vyombo vya habari kama runinga na Radio ambapo matangazo 1,268 ya elimu ya NHIF yalirushwa na makala 52 ziliandikwa magazetini.

Mkurugenzi Mkuu huyo anasema, pia wametoa elimu kupitia mitandao ya kijamii ambapo jumbe za elimu 834 ziliwekwa kwenye mitandao ya mfuko na ya wadau wengine.

Vile vile wamekuwa wakishiriki kwenye maonesho 11 na kutoa elimu kama Sabasaba na Nanenane ambapo watu 17,153 walipewa elimu na watu 4,131 walijiunga na mfuko huo.

"Mfuko ulifanya mikutano 47 na wadau mbalimbali wa mfuko ikiwa ni pamoja na watoa huduma na wanachama katika mikoa mbalimbali."Fahamu kuhusu Kitita kipya cha NHIF>>> 

Jambo lingine ni kuendelea kutekeleza mikakati ya utoaji elimu kwa umma kuhusu dhana na umuhimu wa kuwa na bima ya afya.

"Na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utambuzi, usajili wa wanachama, ukusanyaji wa michango, uwasilishaji, uchakataji na ulipaji wa madai.
"Ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama kwa kuendelea kutoa mikopo ya vifaa tiba, ukarabati, ujenzi na dawa."

Pia, Konga amesema wameendelea kuboresha nuundo wa shirika ili kukidhi mahitaji ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.

“Uhalisia unaonesha kuwa asilimia 85 ya Wananchi hawana Bima ya Afya na hivyo kukosa uhakika wa huduma bora za afya kipindi wanahitaji.”

Amesema, chimbuko la kuandaliwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ni kutimiza wajibu wa Serikali wa kikatiba wa kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila vikwazo

Mbali na hayo pia wameongeza wigo wa mtandao wa vituo vya kutolea huduma za afya kwa kushirikisha wadau mbalimbali nchini.

Ni kwa lengo la kuimairisha uhusiano mwema na wadau wote na kuendelea kuimarisha uhai na uendelevu wa mfuko.

Konga alisema, kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, mfuko huo umepata mafanikio mengi, hivyo mipango waliyonayo ni kuboresha huduma zao na kupata mafanikio makubwa zaidi.

"Hadi kufikia Machi mwakani, mipango yetu ni kuhakikisha tunaongeza idadi ya wanachama sambamba na kuimarisha huduma zetu. Pia, tutahakikisha huduma zinapatikana bila vikwazo na mfuko unakuwa endelevu na unakuwa na ustahimilivu”, alisema Konga.

Aliendelea kusema, mipango mingine waliyonayo ni kuwa Taasisi yenye mchango mkubwa kwa Taifa ikiwemo kukuza uchumi, kwani iwapo wananchi watakuwa na afya njema, watafanya shughuli zao za kujipatia kipato na kuinufaisha nchi.

“Tunataka mwananchi asiuze bodaboda yake au shamba kwa ajili ya kulipia matibabu,” alisisitiza Konga, huku akihimiza wananchi wajiunge na Mfuko huo na wawe tayari kwa Bima ya Afya ya Pamoja.

Alisema, licha ya changamoto iliyopo ya mwamko mdogo wa wananchi kujiunga na bima, lakini wana matumaini makubwa ya kupata wanachama wengi zaidi kutokana na hamasa na elimu wanayoitoa kupitia vyombo vya habari na mitandao mbalimbali ya Kijamii.

“Uhalisia unaonesha kuwa asilimia 85 ya Wananchi hawana Bima ya Afya na hivyo kukosa uhakika wa huduma bora za afya kipindi wanahitaji,” alisema na kuongeza kuwa, chimbuko la kuandaliwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ni kutimiza wajibu wa Serikali wa Kikatiba wa kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila vikwazo.

Maboresho Kitita

Konga amesema,mfuko umeendelea kuboresha kitita chake na unatoa kitita cha mafao chenye wigo mpana ukilinganisha na skimu zingine za bima ya afya (huduma za kibingwa na bobezi).

Amesema,maboresho haya yanatokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika miundombinu na wataalamu katika sekta ya afya nchini.

“Gharama za kugharamia wagonjwa wa saratani kwa mwaka 2023/2023 zilikuwa shilingi bilioni 32.46, ukilinganisha na shilingi bilioni 12.25 mwaka 2021/2022."

Aidha, gharama za matibabu ya figo zilikuwa shilingi bilioni 35.40 na shilingi bilioni 11.45 mtawalia.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, wameimarisha utambuzi wa wanufaika vituoni kwa kutumia alama za vidole na sura (biometric and facial identification).

Pia,kuimarisha mfumo wa TEHAMA kwa kuwezesha wanachama kujisajili, kupata namba ya malipo n.k kwa kutumia mfumo wa kielektroniki (USSD Code *152*00#) na mtandao.

Nyingine ni kuanza kutumia namba za utaifa (NIN) kwa baadhi ya makundi ya wanachama ikiwa ni mbadala wa vitambulisho na kuimarisha utambuzi.

"Na kuweka mfumo wa kushughulikia malalamiko au maoni ya wadau wa mfuko (Customer Relationship Management-CRM).

"Kusogeza huduma karibu na wanachama kwa kuongeza ofisi ndogo za NHIF (Ubungo, Kigamboni na Gongolamboto) ili kusogeza huduma karibu na wananchi."

Amesema, lengo la kufanyika kwa maboresho ni kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa kuzingatia mahitaji halisi ya tiba kwa sasa.

Kuwianisha Miongozo ya Tiba nchini na Kitita cha Mafao na kutekeleza mapendekezo ya Taarifa ya Tathmni ya Uhai wa Mfuko ya mwaka 2021.

Mambo ya msingi yaliyozingatiwa, Konga amesema ni pamoja na kufanya tafiti na uchambuzi wa gharama halisi (costing study) katika soko la huduma za afya nchini.

Ikiwemo kuwezesha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kufanyika katika Hospitali Ngazi ya Kanda kwa maana ya magonjwa ya Moyo, Saratani, Mifupa na mengine.

Sambamba na kuboresha huduma kupitia mikopo kwa watoa huduma."Pia utoaji wa mikopo kwa watoa huduma kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wanachama na wananchi kwa ujumla."Fahamu kuhusu Kitita kipya cha NHIF>>> 

Aina ya mikopo itolewayo, Konga amesema ni ya ujenzi na ukarabati wa majengo,vifaa tiba,vifaa vya TEHAMA na dawa.

Amesema,katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi 2023/24, mfuko huo umetoa zaidi ya shilingi bilioni 24.4 kwa jumla ya vituo 29.

"Tangu kuanzishwa kwa utaratibu huu mwaka 2007, jumla ya vituo 408 vimepokea mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 222.48. "

Ushirikiano

Konga amesema, mfuko umeendelea kupata uzoefu katika namna ya kuhudumia wanachama. Hiyo ni kwa kuzingatia kuwa ni mwanachama wa Umoja wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii Tanzania (TSSA), Umoja wa Mifuko Afrika (ASSA) na Umoja wa Mifuko Duniani (ISSA).

Vile vile wametambulika kutokana na kutoa huduma kwa viwango vya Kimataifa na kupata cheti cha Ithibati (ISO 9001:2015).

Pia,kupata tuzo za Kimataifa katika Ubunifu na Usimamizi bora wa Hifadhi ya Jamii katika maeneo ya TEHAMA na usajili wa wanachama iliyotolewa na ISSA mwaka 2023.

Usimamizi wa rasilimali watu

Konga amesema, hadi kufikia Desemba 2023, mfuko una jumla ya watumishi 697 wanaotekeleza majukumu yao.

Amesema, ni watumishi wenye sifa na weledi katika fani mbalimbali ili kuongeza tija na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Pia, wameweza kujenga uwezo na uzoefu kwa watumishi katika kutekeleza na kusimamia shughuli za bima ya afya kwa umma na kuanza kutekeleza mfumo wa kupima utendaji wa watumishi (PEPMIS).

"Na tumekuwa na mpango endelevu wa mafunzo (Training Programme) na Mkakati wa kuwabakiza kazini (Retention strategy)."

Changamoto

Amesema utaratibu wa malipo ya papo kwa papo na utaratibu wa msamaha husababisha baadhi ya wananchi kukosa huduma kutokana na kukosa fedha za kugharamia huduma za matibabu katika vituo vya kutolea huduma.

Idadi ndogo ya wananchi katika mfumo wa bima ya afya (asilimia 15.3 ya wananchi wote) kutokana na uhiari (NHIF;8%,CHF: 6%, NSSF-SHIB; 0.3% na bima binafsi: 1%).

Pia, amesema, uhiari wa kujiunga na bima ya afya umekuwa ukisababisha wananchi kujiunga wakiwa wagonjwa kinyume na kanuni za bima ya Afya.Fahamu kuhusu Kitita kipya cha NHIF>>> 

Konga, amewaahidi wanachama wa mfuko huo kwamba ifikapo Machi mwakani wanachama watarajie mambo makubwa zaidi ya hayo na kuwataka watanzania kujiunga na mfuko huo Ili wawe na kuhakikisha wa kupata matibabu pindi watakapougua.

TR

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Thobias Makoba amesema, hicho ni kikao cha tatu kwa mwaka huu ambacho kimewakutanisha wahariri na taasisi yakiwemo mashirika umma ambayo yapo chini ya ofisi hiyo.
“Sekta ya Afya imekuwa ni sekta muhimu tangu Uhuru,tutakumbuka Mwalimu (Nyerere) alisema mtu ni afya.

“Na katika wale maadui wanne, maradhi alikuwa namba tatu, sasa kati ya mashirika ambayo yanatusaidia kuepukana, kupiga vita maradhi na kutusaidia kuchochea maendeleo ni shirika (Mfuko) la NHIF."

Amesema, NHIF inasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kama mashirika ambayo hayajiendeshi kibiashara badala yake wanatoa huduma kwa wananchi.

“Katika Sekta ya Afya, NHIF ni moja wapo ya mashirika ya kimkakati katika maendeleo ya Tanzania, kwa sababu huduma wanazozitoa zinagusa moja kwa moja maisha ya Watanzania."

Amesema,ikiwa mwezi huu wa Machi, Serikali ya Awamu ya Sita inaadhimisha miaka mitatu tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan aingie madarakani wameyaomba mashirika na taasisi ambazo zitajitokeza kuelezea mafanikio ambayo wamepata katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news