Wanahabari wanawake mkoani Mara watoa darasa

NA FRESHA KINASA

WANAWAKE nchini wamehimizwa kuendelea kuwa wabunifu na wavumbuzi wa fursa mbalimbali za kiuchumi katika maeneo yao kusudi waweze kuzitumia kikamilifu kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
Hayo yamesemwa Machi 10, 2024, na Mwenyekiti wa Kikundi cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa wa Mara, Jovina Masano wakati akizungumza na Wanawake wa Manispaa ya Musoma katika Uwanja wa Mukendo uliopo Manispaa ya Musoma.
Ikiwa ni sehemu ya muendelezo ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani iliyoadhimishwa Machi 8, 2024 maeneo mbalimbali duniani.
Kikundi cha Waandishi Wanawake kilianzishwa mkoani humo Septemba Mosi, 2023 kwa lengo la kuunganisha nguvu kwa Waandishi wa Habari wanawake waliojikita zaidi kusaidia wanawake ikiwemo kutoa mafunzo yatakayosaidia kujikwamua kiuchumi na kupiga vita ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto mkoani humo.

Jovina amesema kuwa, zipo fursa mbalimbali za kiuchumi zinazowazunguka ambazo bado hazijatumika kikamilifu katika maeneo yao.

Hivyo wakizitumia vyema zitawawezesha kubadilisha maisha yao kiuchumi na kupiga hatua mbele kimaendeleo.
"Tuvumbue fursa mbalimbali za kutuletea maendeleo, kumekuwa na utaratibu wa watu kufanya biashara zinazofanana kwa mazoea bila ubunifu ama ujuzi.

"Lakini kumbe zipo fursa nyingi mpya tunaweza kuzivumbua zikatumika kikamilifu zikaleta maendeleo kiuchumi na kuinua maisha yetu wanawake na familia zetu,"amesema Jovina.

Kwa upande wake Asha Shaban ambaye ni Mwandishi wa Habari wa EATV Mkoa wa Mara amesema kuwa,wanawake wanalojukumu la kuendelea kusimamia malezi bora na maadili mema kwa watoto wao na kujishughulisha katika shughuli za ujasiliamali ili kuwa na kipato.
Aidha, Asha amewataka kutobweteka majumbani badala yake wasimame kidete kupambana na kushirikishana kupeana mbinu na elimu ya ujasiliamali ili waweze kuifanya kwa ufanisi mkubwa.

"Wanawake tutumie nguvu zetu, maarifa yetu na ujuzi kubadilisha maisha ya familia. Tukisimama imara na tukajitambua kisawa sawa tutaweza kuonesha michango na faida yetu kwenye familia yetu na Jamii pia,"amesema Shaban.
Kwa upande wake Ghati Msamba mwandishi wa Gazeti la Uhuru na Katibu wa Kikundi hicho, amesema kuwa, wataendelea kushirikiana na wanawake wote Mkoani humo na kuunganisha nguvu kwa pamoja katika kuhakikisha kwamba wanakuwa hodari na imara katika masuala ya kiuchumi na Kijamii.

"Wanawake tupendane, tujaliane na tushikamane kwa pamoja ili tuweze kwenda mbele. Tusibaguane wala kutengana panapokuwa na fursa zozote zile ambazo zinaweza kutupaisha na kutuneemesha." amesema Msamba.
Naye Rhoda James ambaye ni Mkazi wa Manispaa ya Musoma, amepongeza Waandishi wa Habari wanawake Mkoa wa Mara kwa kuwaunganisha pamoja wanawake wa Manispaa ya Musoma na kushirikiana nao kuelimishana na kupeana mbinu mbalimbali za kimaisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news