Ziara ya Waziri Mkuu yawaamsha wadau Musoma Vijijini mapambano dhidi ya uvuvi haramu

NA FRESHA KINASA

IMEELEZWA kuwa, ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa aliyoifanya Musoma Vijijini Machi 29, 2024 imetoa hamasa na ushawishi mkubwa kwa wavuvi katika Jimbo la Musoma Vijijini kuachana na uvuvi haramu.
Wakati wa hotuba yake akiwa Musoma Vijijini katika Kijiji cha Bwai Kwitururu, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, aliwataka wavuvi kuachana na uvuvi haramu, kwani athari yake ni kubwa na pia Serikali imetoa katazo juu ya uvuvi huo.

Alisema, wavuvi wanapaswa kufanya uvuvi ulioruhusiwa kisheria na kutumia zana ambazo hazina athari.

Huku akiomba maafisa uvuvi, viongozi wa Serikali za mitaa na wananchi kwa ujumla kuwafichua mbele ya sheria wanaofanya uvuvi haramu, kwani umepigwa marufuku kisheria.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema, kwa kutambua umuhimu wa sekta ya uvuvi katika kuleta maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla, Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikitoa zana bora na za kisasa kwa wavuvi ili wafanye kazi hiyo kwa ufanisi na pia serikali inahamasisha wavuvi waunde vikundi kuweza kusaidiwa mikopo na elimu ya uvuvi endelevu usio na athari.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Machi 6, 2024 imeeleza kuwa, "Kufuatia ziara ya Waziri Mkuu Majaliwa, wadau wa maendeleo wa Jimbo la Musoma Vijijini wanashirikiana na Serikali yetu kutokomeza uvuvi haramu ndani ya Ziwa Victoria,"imeeleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza kuwa.

"Mmoja wa wadau ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Wilaya ya Musoma Vijijini, ndugu Jackson Nyakia Kikomati ambaye anaunga mkono kutokomeza uvuvi haramu kwa kusaidia mitumbwi wavuvi ili waachane na uvuvi haramu.

"Na wafanye uvuvi endelevu ambao pia utasaidia Serikali kupata mapato na wavuvi kunufaika kwa kupata kipato halali."

Wananchi nao kwa upande wao, wanaunga mkono kauli ya Waziri Makuu Majaliwa na kuahidi kuachana na uvuvi haramu ambapo wamesema unarudisha nyuma maendeleo na kuleta athari kwa rasilimali zilizoko ndani ya Ziwa Victoria.

Juma Costantine ambaye ni mvuvi katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma amemshukuru Prof. Muhongo kwa jinsi ambavyo amekuwa akisisitiza wavuvi kutojihusisha na uvuvi haramu na kuomba serikali kuwezesha wavuvi wafuge kwa vizimba, hali ambayo imechangia baadhi ya wavuvi kunufaika na fursa zinazotolewa na Serikali kwa sekta ya uvuvi jimboni humo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news