Rhobi Samwelly awawezesha vifaa vya kujifunzia wanafunzi wenye mahitaji maalum

NA FRESHA KINASA

MKURUGENZI wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly amekabidhi vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanaosoma katika Shule ya Msingi Butiama 'A' iliyopo Wilaya ya Butiama.
Vifaa hivyo ni pamoja na Tv ya kisasa, spika, king'amuzi cha Azam kwa ajili ya kutazama taarifa ya habari na maiki vikiwa na thamani ya shilingi milioni 1.5. Ambapo vitaweza kuwasaidia wanafunzi hao wenye mahitaji maalumu wakiwemo viziwi, watoto wenye mtindio wa ubongo, watoto wenye uoni hafifu.

Rhobi amekabidhi vifaa hivyo Machi 6, 2024 akiwa ameongozana na viongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Butiama.
Ambapo, jumuiya hiyo imeadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kugawa mahitaji mbalimbali ikiwemo kalamu, daftari, taulo za kike, sabuni na mafuta ya kupaka katika shule za Msingi Butiama A, Shule ya Sekondari Butiama, Shule ya Msingi Bumaswa na kutembelea kituo cha afya Kiagata na kugawa mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa.

"Nilipokea maombi uongozi wa shule wakiniomba vifaa hivi kusudi viwasaidie wanafunzi wenye mahitaji Maalumu shileni hapa. Nami kwa kutambua umuhimu na thamani ya elimu nimeleta vifaa hivi naamini kabisa vitakuwa na msaada mkubwa kwa wanafunzi hawa ambao ni tegemeo kwa Taifa letu."amesema Rhobi.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika shule hizo, Rhobi amewataka wanafunzi hao wajitambue na wasome kwa bidii kuhakikisha ndoto zao zinatimia. Kwani serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeboresha miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na kujenga vyumba vya madarasa ili kila mtoto apate fursa ya elimu bila malipo.

Pendo Wambura ni Mwalimu wa Kitengo cha Wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Butiama 'A' amemshukuru Rhobi Samwelly kwa kutoa vifaa hivyo ambapo amesema, vitawezesha wanafunzi hao kusoma vizuri tofauti na awali.
"Shule hii inajumla ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu wapatao 52, wapo viziwi, wenye mtindio wa ubongo, wenye uoni hafifu na Walemavu. Tumeomba vifaa hivi muda mrefu kwa watu mbalimbali bila mafanikio. Tunamshukuru sana Rhobi kwa kuguswa kutusaidia baada ya kumuomba, Mungu ambariki sana kwa kuguswa hitaji kubwa la Watoto hawa." amesama Pendo.

Naye Jane Mbura ambaye ni Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Butiama amesema kuwa Jumuiya hiyo imeamua kutumia maadhimisho ya siku ya Wanawake ambayo huadhimishwa Machi 8, kila mwaka kutoa mahitaji mbalimbali kwa wanafunzi pamoja na mahitaji kwa wagonjwa Katika kituo cha afya Kiagata.
Amesema,jumuiya hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na wadau mbalimbali wanaopambana na vitendo vya ukatili wa Kijinsia na kuimarisha haki za binadamu ili kujenga usawa katika jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news