Benki ya TCB kuwaneemesha wajasiriamali mbalimbali nchini

NA GODFREY NNKO

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imesema, mwaka huu itatoa mikopo ya shilingi bilioni 300 ili kuinua uchumi wa nchi hasa kwa wajasiriamali mbalimbali.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Bw. Adam Mihayo (kulia), akijadili jambo na Bw. Sabato Kosuri, kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Afisa Mtendaji Mkuu, Adam Mihayo ameyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri wakiwemo waandishi wa habari chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Mihayo amesema benki hiyo ambayo mwakani inafikisha miaka 100 tangu kuanzishwa mwaka 1925, imepitia mengi inagawa sasa inaendelea vizuri na pamoja na mikopo hiyo.

Pia, amesema imedhamiria ndani ya miaka mitatu kushika nafasi ya tatu kwenye taasisi za fedha nchini.

Mihayo amesema, TCB inahudumia Watanzania wa makundi zaidi ya milioni mbili, hivyo ili kufanikisha lengo la kukua kibiashara na huduma, mwaka huu itatoa mikopo ya shilingi bilioni 300 kwa wafanyabiashara na wajasiriamali 2,000.

“TCB tumejipanga kuchangia ukuaji uchumi na biashara kwa kufikia watu wengi hasa wajasiriamali.

"Lakini pia tunarajia faida ya benki yetu kabla ya kodi itaongezeka hadi shilingi bilioni 40 na hilo limeoneka, kwani katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 tumepata faida ya zaidi ya shilingi bilioni 10 kutoka shilingi bilioni 3 robo ya kwanza ya mwaka 2023,” amesema.

Amesema, dhamira ya TCB kuwa benki namba tatu kwa ukubwa nchini, itafanikiwa kwani inafikia watu wengi wanaohitaji huduma za kibenki, hivyo kuomba Watanzania kuitumia ili kunufaika kiuchumi.

Mihayo amesema hadi sasa TCB ina matawi 82, ATM 1,031, wakala 6,000 ikiwa ni ongezeko la wakala 4,416 na mipango yao ni kuongeza wakala hadi 10,000 na huduma zao zimejiunga na Mkoba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news