DCEA yakamata kilo 54,489.65 za dawa za kulevya, watuhumiwa 72

DAR ES SALAAM-Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ikiwemo Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) imekamata kilo 54,506.553 za dawa za kulevya wakiwemo watuhumiwa 72.
Ni kupitia operesheni iliyofanyika katika mikoa ya Shinyanga, Tabora, Iringa, Mbeya, Arusha na Dar es Salaam.

Dawa hizo zinajumuisha za mashambani na viwandani pamoja na kuteketeza ekari 262 za mashamba ya bangi.

Hayo yamesemwa leo Aprili 4,2024 na Kamishna Jenerali wa DCEA,Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar Es Salaam.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema, dawa zilizokamatwa ni bangi kilo 54,489.65, mirungi Kilogramu 10.3, heroin gramu 90.93 na cocaine gramu 1.98.

Nyingine ni kilogramu 4.623 za aina mpya ya dawa ya kulevya inayoitwa methylene dioxy pyrovalerone (MDPV) iliyokamatwa jijini Dar es Salaan ikisafirishwa na raia wa Comoro anayeitwa Ahmed Bakar Abdou (32).
"Watuhumiwa 72 wamekamatwa kuhusika na dawa hizo na baadhi yao tayari wamefikishwa mahakamani.

"Methylene dioxy pyrovalerone (MDP) ni dawa mpya ya kulevya iliyo katika kundi la vichangamshi inayotengenezwa kwa kutumia kemikali bashirifu."
Amesema, dawa hiyo ina kemikali inayoweza kuleta madhara ya haraka kwa mtuniaji ikilinganishwa na dawa nyingine za kulevya.

Pia, imeongezwa nguvu ya kilevi inayozidi cocaine, heroin na methamphetamine.

"Aidha, dawa hii ya kulevya huuzwa kwa njija ya mtandao (internet) na husafirishwa kupitia kampuni za usafirishaji vifurushi na hufichwa kwa kuwekwa chapa za majina bandia kama vile bath salts, Ivory Wave, plant fertilizer, Vanilla Sky, na Energy."

Vile vile, amesema Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imebaini uwepo wa mashamba makubwa ya bangi katika hifadhi za misitu ya Ubangu mkoani Shinyanga na Mabatini mkoani Tabora ambapo wahalifu hao wamekata miti katikati ya misitu hiyo na kulima bangi.
"Kwa ushirikiano tulioupata kutoka kwa Wakala wa Misitu (TFS) tulifanikiwa kuteketeza mashamba hayo na kuwakamata wahusika.

"Tunatoa shukrani zetu kwa wananchi kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu wazalishaji na wauzaji wa dawa za kulevya katika maeneo yao na tutaendelea kushirikiana na wadau na jamii kwa ujumla ili kufanikisha operesheni zetu.

"Hivyo, tunaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa Mamlaka,"amefafanua Kamishna Jenerali Lyimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news