Fahamu, kwa nini BoT imeweka mkazo Elimu ya Fedha ifundishwe ngazi zote za elimu

NA GODFREY NNKO

NAIBU Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Omary Kipanga amefungua warsha ya siku tatu ambayo inaangazia namna ya kuingiza Elimu ya Fedha katika mitaala ya elimu ya juu nchini.
Warsha hiyo ambayo inawakutanisha wadau mbalimbali kutoka taasisi za elimu ya juu nchini imeanza leo Aprili 17, 2024 na inafanyika katika makao makuu ndogo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam. 

Aidha, imeandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Kipanga akifungua warsha hiyo amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imedhamiria kujenga uelewa wa masuala ya fedha kwa wananchi wote.

Amesema, wizara hiyo itahakikisha elimu ya fedha inafundishwa katika mfumo wa elimu nchini. “Kutokana na mabadiliko makubwa na ya haraka ya Sekta ya Fedha,ni vema jamii nayo ikashiriki kuchangia upatikanaji wa mabadiliko hayo ili iweze kufaidika na huduma zitakazotolewa.”

Mheshimiwa Kipanga amesema, kukosekana kwa uelewa wa masula ya fedha kwenye jamii ni sababu kubwa inayozorotesha biashara zinazoanzishwa.

“Biashara nyingi haziwezi kukuwa na zikaendelea kizazi hadi kizazi. Kila kizazi kinaanzisha biashara mpya ambayo nayo inakufa baada ya yule aliyeanzisha kuondoka.

“Hivyo twende kwa haraka kuhakikisha vijana ambao ni sehemu ya jamii nchini wanakuwa na uelewa wa masuala ya fedha, ninatarajia wakuu wa vyuo mtabeba uelewa huo muhimu kwa vyuo vyetu nchini.

“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ipatiwe taarifa ya tathmnini mtakazofanya ili itusaidie katika kufanya maamuzi, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kujenga uelewa wa masuala ya fedha kwa jamii,” amesema Mheshimiwa Kipanga.
Naibu Waziri huyo amesema, Benki Kuu itaendelea kusimama na vyuo na taasisi za elimu na Wizara ya Elimu katika kuhakikisha dhana ya elimu hiyo inakuwa endelevu na inafundishwa katika ngazi za jamii hata katika elimu zisizo rasmi nchini.

Awali, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha Sauda Msemo amesema, warsha hii ya siku tatu ni muhimu katika kuendeleza jitihada za ushirikiano ulioanza tangu mwaka 2023 kati ya Benki Kuu ya Tanzania na Wizara ya Elimu na Teknolojia

Msemo amefafanua kuwa, ushirikiano huo umedhamiria kuhakikisha kuwa, elimu ya fedha inatolewa kwa vijana wote kutoka elimu awali hadi elimu ya juu nchini.

"Lengo kuu la siku tatu hizi ni kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kuhakikisha elimu ya fedha inakuwa sehemu ya mitaala ya elimu ya juu nchini.

"Na namna bora ya kufundisha somo hili, ili liweze kuwapatia ujuzi wanafunzi wa vyuo vikuu kuweza kusimamia fedha binafsi."

Amesema, mkusanyiko huo unathibitisha dhamira ya thati ya elimu nchini kuendelea kushirikiana katika kutimiza lengo la kuhakikisha elimu ya fedha inakuwa sehemu ya masomo katika mfumo wa elimu na ifundishwe kwa wanafunzi wa ngazi zote.

Pia, BoT imeishukuru Wizara ya Elimu kwa kuhakikisha suala la Elimu ya Fedha linapewa uzito kuanzia elimu ya wali nchini.

Naibu Gavana huyo amesema, tayari somo hilo limechopekwa (limeingizwa) katika mfumo wa elimu ya msingi na sekondari kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania.

“Mwezi Aprili, mwaka jana Benki Kuu ya Tanzania iliwashirikisha wakuu wa taasisi za elimu ya juu hapa nchini kwa uwakilishi wa vyuo vikuu pamoja na TCU na NACTVET kwa lengo la kukubaliana juu ya azima ya kufundisha somo la elimu ya fedha katika vyuo vikuu nchini.

“Hadi sasa, taasisi tatu za elimu ya juu zimechukua hatua ya kuingiza elimu ya fedha katika mitaala yao na warsha hii ni sehemu ya kuchochea uingizwaji wa wa elimu ya fedha katika mitaala ya elimu ya juu nchini kwa vyuo vingi.Na hatimaye vyuo vyote nchini viweze kuwa na mitaala inayohusisha elimu ya fedha."

Vile vile, amesema fursa iliyotolewa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa ajili ya Mageuzi ya Kiuchumi itawezesha azima hii ya kuongeza taasisi za elimu ya juu zilizoweza kuwa na elimu ya fedha katika mitaala yao ili kukabiliana na mabadiliko ya mazingira ya fedha kwa sasa.

"Kama tunavyojua, idadi kubwa ya Watanzania ni vijana,na takwimu za Sensa ya mwaka 2022 zinaonesha kuwa, takribani asilimia 34.5 ya idadi ya watu nchini wana umri wa miaka kati ya 15 hadi 35.

"Hivyo ili kuleta tija na ufanisi katika masula ya uchumi ni dhairi kuwa, ujuzi na uzoefu wa elimu ya fedha ni moja ya sifa muhimu kufikia azima hiyo kwa Taifa lolote.

"Kutoa elimu ya fedha kwa Watanzania walio wengi itachochea maendeleo kwa kuongeza utumiaji wa huduma rasmi za fedha na kuwawezesha watu wengi kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kuendesha shughuli zao mbalimbali kwa ufanisi zaidi na kukuza uchumi kwa ujumla."

Pia, Naibu Gavana huyo amesema, matarajio ya siku hizo tatu ni kuhakikisha mitaala ya somo la elimu ya fedha linazingatiwa.

"Ni ili kuwawezesha vijana waliopo katika elimu ya juu kuwa na uwezo wa kuelewa na kusimamia masuala ya fedha ikiwemo kujipatia kipato halali."

Pia, kuweka akiba, kupanga bajeti, kuweka mipango, kufanya uamuzi wa masuala ya fedha kwa kuzingatia viashiria hatarishi na kuelewa taasisi mbalimbali zinazotoa huduma ya fedha.

“Ili kufanya maamuzi ya kifedha sahihi, tunategemea kwamba,elimu hii itakapokuwa inafundishwa vijana wa elimu ya juu, vijana hao au wanafunzi hao wataweza kutawala fedha na siyo fedha iwatawale.
“Tunafahamu huwa inatokea mtu mwingine akishapokea boom hivi au fedha zingine zozote, tunasema boom kwa sababu ya wanafunzi zaidi, unakuta kwamba mambo mengine yote yanasimama.Kwa hiyo tunategemea kujenga nidhamu kupitia elimu ya fedha.”

Kuhusu Watanzania ambao wapo nje ya mfumo wa elimu nchini ambao kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022 inaonesha asilimia 53.4 wapo katika umri wa kufanya kazi kuanzia miaka 15 hadi 64 amesema,

“Hivyo, Benki Kuu kwa kushirikiana na wadau wengine wa Baraza la Huduma Jumuishi la Fedha imetoa muongozo na mtaala wa elimu ya fedha kwa wakufunzi ambao utatumika na taasisi za elimu ya juu kwa kuwafundisha watoa huduma za elimu ya fedha kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi nchini walio nje ya mfumo rasmi wa elimu.

“Tayari tuna ushirikiano yaani Memorandum of Understanding na baadhi ya taasisi za elimu katika utekelezaji wa mtaala huu wa wakufunzi wa elimu ya fedha.”

Amesema, taasisi hizo ni Chuo Kikuu cha Iringa, Chuo Kikuu Zanzibar, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania.“Tunakaribisha vyuo vingine pia, kuunga mkono jitihada hizi.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news