🔴LIVE:Serikali mbioni kuhuisha Sera ya TEHAMA ya mwaka 2016 kuchagiza uchumi wa kidigitali

ARUSHA-Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama nchini, Dkt.Nkundwe Moses Mwasaga amesema, kwa sasa Serikali ipo mbioni kuhuisha Sera ya TEHAMA ya mwaka 2016 ili iweze kuchagiza ukuaji wa uchumi wa kidijitali kwa kasi zaidi.
Dkt.Mwasaga ameyama hayo leo Aprili 4, 2024 jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Tatu la Usalama wa Mitandao likiongozwa na kauli mbiu ya ‘Kutengeneza Dunia ya mtandao iliyo jumuishi na shirikishi’.

“Kama mnavyofahamu na baadhi yenu mmeshirikishwa, wizara yangu (Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) hivi sasa inaendelea kuhuisha Sera ya TEHAMA ya mwaka 2016 ili iweze kuchagiza ukuaji wa Uchumi wa kidijitali kwa kasi zaidi.”

Pia, amesema mwaka 2022, Bunge limepitisha Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na kupitia sheria hiyo tayari imeanzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

“Tunaendelea kufanya mapitio ya sheria zetu mbalimbali katika sekta ya TEHAMA ili ziweze kuendana na ukuaji wa teknolojia za kidijitali.
“Hivyo, niendelee kuwasihi kuwa Serikali iko tayari kuendelea kushirikiana nanyi pamoja na wadau wote kutatua changamoto zote hususani za usalama wa miundombinu ya TEHAMA pamoja na matumizi salama ya huduma za kidijitali.

“Ninaamini kupitia jukwaa hili tutapokea mawazo na maoni mbalimbali ya maeneo ya kisera na kisheria yanayohitaji kuboreshwa zaidi ili kuendelea kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa katika nafasi salama ya ulimwengu wa kidijitali. “

Amesema, mikutano ya aina hii ni chachu kubwa ya kuendelea kuhamasishana, kukumbushana na kubadilishana uzoefu na mawazo juu ya hatua stahiki ambazo zinapaswa kuchukua ili kuwa na Dunia salama katika ulimwengu wa kidijitali.

Dkt.Mwasaga amefafanua kuwa,katika ulimwengu wa sasa, mageuzi ya kidijitali ni nguzo kuu ya kuwezesha uchumi wa kidijitali.

“Mageuzi haya ya kidijitali yanajengwa na msingi wa dhana kuu mbili. Kwanza ni kutumia teknolojia za kidijitali yaani digitization katika shughuli zetu ili kuongeza ufanisi, mapato na hata kukuza ubora wa bidhaa na huduma mbalimbali.

“Dhana ya pili ni mabadiliko ya tabia za binadamu yaani change of human behavior. Dhana hii ya pili inalenga kuhakikisha kuwa binadamu ambao ni watumiaji wa huduma za kidijitali na walaji wa huduma na bidhaa zitokanazo na TEHAMA wanakuwa na utayari wa kutumia TEHAMA ili kuleta mabadiliko na kuongeza ufanisi katika shughuli za kila siku.”

Dkt.Mwasaga ameongeza kuwa, dhana hizi mbili haziwezi kufanikiwa endapo mifumo ya kidijitali itatishia usalama wa nchi, itakuwa kikwazo kwa ukuaji uchumi, itatishia ukuaji wa biashara za makampuni na zile shughuli za mtu mmoja mmoja.

Pia kutokuwepo kwa matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali kunaweza kupelekea kutwezwa kwa utamaduni wa taifa na utu wetu kwa kuruhusu taarifa za siri za Serikali, kampuni na hata zile za mtu binafsi kupatikana kwa utaratibu usio sahihi na kutumiwa na watu wasiokuwa na dhamana ya kutumia taarifa husika.

“Hivyo, malengo ya mageuzi ya kidijitali hayawezi kufikiwa endapo suala la usalama wa mitandao linalowezesha matumizi salama ya huduma za kidijitali halitapewa uzito unaoendana na kasi ya maendeleo ya TEHAMA.”

Amesema, kwa kutambua umuhimu wa kuhakikisha kuwa Tanzania iko katika nafasi salama katika ulimwengu wa kidijitali,ndiyo maana Tume ya TEHAMA ambayo ina jukumu la msingi la kukuza maendeleo ya TEHAMA imeona ni vema wadau wote wakutane kwa siku mbili ili kufanya
tathmini ya utekelezaji wa mikakati mbalimbali na kutoa ushauri.

Sambamba na mwelekeo wa matumizi salama ya mitandao ya kompyuta na huduma za kielektroniki kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news