Naibu Waziri Pinda amshukuru Rais Dkt.Samia ujenzi njia ya umeme Mpimbwe

NA MUNIR SHEMWETA

MBUNGE wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Geophrey Pinda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji mradi wa ujenzi wa njia ya umeme kutoka Inyonga hadi Majimoto katika Halmashauri ya Mpimbwe Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi.
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda (Katikati) akimsikiliza Meneja wa TANESCO wa wilaya ya Mlele Zebron Malima (kushoto) alipokwenda kukagua nguzo za umeme zitakazotumika kwenye mradi wa ujenzi wa njia ya umeme kutoka Inyonga hadi Majimoto katika halmashauri ya Mpimbe tarehe 10 April 2024. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI).

Halmashauri ya Mpimbwe kwa sasa inapokea umeme kutoka Zambia ambao umeelezwa kukatika mara kwa mara kunakosababishwa na radi zinazopiga nguzo za umeme kwenye milima Lyambalyamfika inayotenganisha mkoa wa Rukwa na Halmashauri ya Mpimbe.

"Mama tunakushukuru sana sisi wananchi wa Mpimbwe na Mlele. Pia nimshukuru Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Mpango alipotembelea kituo cha umeme Mlele alitoa maelekezo kuwa njia ya umeme kutoka Inyonga kwenda Majimoto ijengwe. Nashukuru sana na huo ni ushahidi tosha kwamba sasa kazi imeanza utekelezaji,"amesema Mhe. Pinda.
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akikagua nguzo za umeme zitakazotumika katika mradi wa ujenzi wa njia ya umeme kutoka Inyonga hadi Majimoto katika halmashauri ya Mpimbe tarehe 10 April 2024.

Akizungumza wakati wa kukagua nguzo za umeme kwa ajili ya utekelezaji mradi huo katika wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi tarehe 10 April 2024, Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema, uamuzi wa serikali kujenga njia ya umeme siyo tu utawasaidia wananchi na wafanyabiashara bali utachochea shughuli za maendeleo kwenye halmashauri ya Mpimbwe hususan wananchi wa jimbo lake la Kavuu.

Amebainisha kuwa, wananchi wa Mpimbwe wamekuwa wakipata shida ya huduma ya umeme alioueleza kuwa unakatika mara kwa mara na hivyo kuwafanya kushindwa kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

Amewataka wananchi wa jimbo lake la Kavuu kuwa na subira wakati mradi huo ukitekelezwa huku akiwaeleza kuwa, mambo mazuri hayahitaji haraka na kusisitiza kuwa, mradi huo ni sehemu ya mafanikio makubwa ya jimbo na ni eneo ambalo serikali imelipa umuhimu wa pekee katika kusimamia na kuwaletea wananchi huduma mbalimbali kama vile umeme.
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda (wa pili kushoto) akisindikizwa na Mkuu wa Wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Alhaji Majid Mjengwa (wa kwanza kulia) pamoja na Meneja wa TANESCO wilaya ya Mlele Zebron Malima kwenda kukagua nguzo za umeme zitakazotumika kujenga njia ya umeme kutoka Inyonga hadi Majimoto katika halmashauri ya Mpimbe tarehe 10 April 2024.

"Wafanyabiashara wenye mashine za kukoboa mpunga na mazao memgine ya chakula wawe watulivu na baada ya miezi michache ni kama opereshemi ya miezi miwili tutakuwa tuna umeme, utakapowashwa ule wa gridi ya taifa maana yake utawashwa mpaka jimbo la Kavuu ambalo kadhia ya umeme inaenda kumalizika,"alisema.

Mkuu wa wilaya ya Mlele, Alhaji Majid Mjengwa alimueleza Mheshimiwa Pinda kuwa, tayari wameanza kupokea nguzo kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa njia ya umeme kutoka Inyonga hadi Majimoto halmashauri ya Mpimbwe wenye urefu wa takriban kilomita 135 ambapo ameelezea hatua hiyo ni faraja kwao na wananchi wa jimbo lake la Kavuu kwa ujumla.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Mlele ameweka wazi kuwa, wao kama wasimamizi wa mradi watahakikishia mahitaji yote muhimu kama vile ulinzi kwa watakaofanya kazi kipande chote cha hifadhi unaimarishwa.

"Mahitaji yote kama kuhakikisha askari wa TAWA na wale wa wanyama pori wanakuwepo kutoa ulinzi kwa watakaofanya kazi kipande cha hifadhi, tutashirikiana nao kwa maana ya mkandarasi kuhakikisha hawakwami na tuko tayari kutoa usaidizi utakaohitajika.
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda (Katikati) akiangalia nguzo za umeme zitakazotumika kujenga njia ya umeme kutoka Inyonga hadi Majimoto katika halmashauri ya Mpimbe tarehe 10 April 2024.

"Tutahakikisha wanaofanya kazi hawakwami katika kipande chote cha hifadhi na sisi kama wasimamizi tutatoa usaidizi kutoka askari wa hifadhi pamoja na wale wa TAWA hawakwami,"alisema Alhaji Mjengwa.

Mradi wa Ujenzi wa njia ya umeme wa Inyonga hadi Majimoto unaoenda sambamba na ule wa Gridi ya Taifa kutoka Tabora umeelezwa kuwa suluhusho la kukatika kwa umeme mara kwa mara na hivyo kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara zao za kusindika mazao bila wasiwasi wowote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news