Serikali, wadau kuja na ufumbuzi ajali za usafiri wa vyombo vidogo vidogo majini

NA GODFREY NNKO

SERIKALI imesema, jitihada mbalimbali zinaendelea kufanyika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha ajali zinazotokea katika usafiri wa majini kupitia vyombo vidogo vidogo zinadhibitiwa.
Hayo yamesemwa leo Aprili 16, 2024 na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano, na Uchukuzi Zanzibar,Mhe. Khalid Salum Mohamed wakati akifungua Semina ya Usalama wa Vyombo vya Usafirishaji katika Kanda ya Afrika inayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Semina hiyo ya siku mbili imeandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),International Marinetime Organisation (IMO) na Interferry.

Lengo la semina hiyo ni kutoa fursa kwa wadau mbalimbali kujadili mbinu bora za kuboresha Usalama wa Vyombo vya Usafiri Majini barani Afrika.

Akifungua semina hiyo maalum kwa wadau ambao wanaotumia vyombo vidogo vidogo kusafirisha abiria katika maeneo ya mwambao mwa nchi za Afrika, Waziri Mohamed amesema, inafanyika kwa kipindi mwafaka ambapo washiriki wanatakuja na suluhusho la ajali hizo.

Amesema, mkutano huo umewaleta pamoja kwa sababu inaonekana eneo hilo halijapewa mkazo unaostahili.

"Mkazo mkubwa upo katika meli ambazo zinasafiri kwenda katika bahari kuu na siyo feri boti ambazo tunasafiria katika mwambao wetu. Kwa mfano unatoka Zanzibar unakuja Dar es Salaam, unakwenda Tanga, unakwenda Mombasa hizi hazijapewa ule mkazo ambao unastahili.

"Lakini, kwa ujumla inaonekana kwamba ajali nyingi sana zinatokea katika vyombo hivyo. Na ajali hizo zinasababisha maafa makubwa, vifo, watu kuumia lakini pia na mali kupotea."

Waziri huyo amesema,miongoni mwa sababu zinazochangia ajali nyingi za majini ndani na nje ya Tanzania ni pamoja na utendakazi usioridhisha wa waendeshaji wa boti na vivuko.

Pia, wakati mwingine ni wafanyakazi, wasimamizi wa vituo na wasafiri wa baharini, usanifu mbaya wa vyombo vya usafirishaji majini, hali mbaya ya hewa ikiwemo ukosefu wa vifaa vya usalama vya kutosha kwa ajili ya uokoaji.

Amesema, ili kukabiliana na changamoto hizo, nchi za Afrika zinapaswa kuimarisha hatua za usalama na kuweka mifumo ya usimamizi wa usalama ambayo inahakikisha usalama wa vyombo vya usafirishaji majini na kuzuia ajali hizo.

"Nchi nyingi barani Afrika zinategemea sana usafiri wa baharini kwa kuunganisha maeneo na watu. Kwa hiyo, sekta hii ina jukumu kubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya bara letu.

"Usafiri wa majini katika visiwa kama vile Zanzibar, Comoro, Mauritius na Sao Tome & Principe ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafiri zinazohudumia wenyeji na watalii.

"Pia ni njia muhimu katika nchi zenye mifumo mikubwa ya mito na maziwa makubwa kama vile Tanzania Bara, Kenya, Zambia, Uganda, Msumbiji, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Nigeria."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news