Serikali yakamilisha Kinyerezi I Extension MW 185

NA GODFREY NNKO

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko amesema, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imekamilisha ujenzi wa mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi I Extension MW 185 ambapo kwa sasa mitambo yote minne inafua umeme.
Dkt.Biteko ameyasema hayo leo Aprili 24, 20024 wakati akiwasilisha bungeni jijini Dodoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

"Aidha, hadi kufika Machi 2024, kazi ya upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Kinyerezi ulikuwa imefikia asilimia 97.6 ambapo transfoma mbili zenye uwezo wa MVA 175 zilikuwa zimefungwa kwenye misingi yake na ujenzi wa barabara, ufungaji wa taa na mifumo ya ulinzi ulikuwa unaendelea."

Vilevile, Dkt.Biteko amesema, vituo vya Mbagala na Gongolamboto vinaongezewa uwezo kufikia MVA 170 kutoka uwezo wa awali wa MVA 50.

Pia, amefafanua kuwa, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 19.2 ya msongo wa Kilovoti 132 kutoka Kinyerezi hadi Mbagala kupitia Gongolamboto jijini Dar es Salaam umefikia asilimia 55.

Kwa mwaka wa fedha ujao, Mheshimiwa Dkt.Biteko ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liidhinishe bajeti ya wizara hiyo ambayo ni zaidi ya shilingi trilioni 1.883 kwa ajili ya matumizi ya wizara na taasisi zake.

Dkt.Biteko amesema, kupitia fedha hizo,shilingi trilioni 1.794 sawa na asilimia 95.28 ya bajeti yote ya wizara ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Aidha, kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 1.54 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 258.85 ni fedha za nje huku shilingi bilioni 88.89 sawa na asilimia 4.72 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

"Kati ya fedha hizo shilingi bilioni sitini na tisa, milioni mia tano ishirini na nne, mia mbili na moja elfu (shilingi 69,524,201,000) ni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC)."

Ameongeza kuwa,shilingi bilioni 19.37 ni kwa ajili ya Mishahara (PE) ya watumishi wa wizara na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news