TASAC yafafanua kuhusu kupotea Jahazi la mizigo likiwa na tani 65 za mbao

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema kuwa, Jahazi la mizigo liitwalo MV TAWAKAL III limepotea likiwa na tani 65 za mbao.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 23,2024 na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mohamed Malick Salum.

"Mnamo tarehe 20 Aprili 2024 majira ya saa 11:00 jioni, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kupitia Kituo cha Kuratibu Utafutaji na Uokoaji (MRCC) lilipokea taarifa ya kupotea kwa Jahazi la mizigo liitwalo MV TAWAKAL III.

"Baada ya ufuatiliaji wa karibu juu ya taarifa hiyo, TASAC ilibaini kuwa Jahazi hilo limesajiliwa na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (Zanzibar Maritime Authority-ZMA) kwa namba za usajili Z-1430,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu wa TASAC kupitia taarifa hiyo.

Amebainisha kuwa,TASAC ilichukua hatua za haraka za kuwasiliana na kuratibu zoezi la utafutaji na hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kuwezesha upatikanaji wa jahazi hilo ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na mamlaka mbalimbali za Serikali na wadau.

"Aidha, taarifa zimepelekwa katika mamlaka zilizo nchi jirani za Kenya na Visiwa vya Komoro ambapo ndio maeneo ambayo upo uwezekano wa Jahazi hilo kuwa limesukumwa na upepo katika uelekeo wa nchi hizo.

"Aidha, Jahazi hilo liliondoka katika Bandari ya Kilwa Kivinje majira ya saa 7:00 mchana mnamo tarehe 19 Aprili 2024 na lilitarajiwa kuwasili katika Bandari ya Malindi mjini Zanzibar tarehe 20 Aprili 2024 majira ya saa 8:00 mchana."

Kwa mujibu wa taarifa hiyo,jahazi hilo lenye urefu wa mita 17 likiwa na mabaharia (wafanyakazi) watano (5) raia wa Tanzania lilisheheni tani 65 za mzigo wa mbao na hakukuwa na abiria.

"Hadi kufikia tarehe 23 Aprili 2024, hakuna dalili zozote za kuonekana au kupatikana kwa wafanyakazi wake watano (5) au “MV TAWAKAL III”.

"TASAC inaendelea na uratibu wa utafutaji na kuahidi kuendelea kutoa taarifa mpya kwa umma kadri zinavyopatikana.

"TASAC inaendelea kushukuru juhudi za pande zote zinazohusika na linawaomba wananchi na wadau kutoa taarifa zozote zinazoweza kusaidia kupatikana kwa wafanyakazi wake na Jahazi hilo.

"Toa taarifa katika Kituo cha Kuratibu Utafutaji na Uokoaji (MRCC) kupitia namba ya bure bila: +255 80 011 0101 au barua pepe: mrccdar@tasac.go.tz,"ameeleza Mkurugenzi Mkuu kupitia taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news