Timu zinapendelewa, nyumbani na ugenini

NA LWAGA MWAMBANDE

APRILI 5,mwaka huu wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika kwa maana ya Yanga SC na Simba SC walishuka dimbani kwa nyakati tofauti.
Ni mitanange ambayo pia ilipigwa katika mataifa tofauti kwa maana ya Simba SC kumenyana na Al Ahly ndani ya Uwanja wa Cairo International nchini Misri ambapo walipoteza kwa mabao 2-0.

Kwa upande wa watani zao Yanga SC dakika tisini walitoka sare ya 0-0 na Mamelodi Sundowns katika dimba la Loftus Versfeld jijini Pretoria, Afrika Kusini.
Baadaye penalti zikaamua mshindi ingawa uamuzi wa Refa Dahane Beida wa Mauritania ambaye alilazimika kutumia Teknolojia ya VAR dakika ya 58 kuamua juu ya shuti la kiungo mshambuliaji wa Yanga,Stephanie Aziz Ki aliibua maswali ambayo yamesababisha wengi kutoridhika.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande kutokana na changamoto hiyo, leo ameibua hoja hii. Endelea;

1.Timu zinapendelewa, nyumbani na ugenini,
Hili twapaswa elewa, au tunangoja nini,
Watu wamefanyiziwa, hii wala si amani,
Magoli yawe ya kweli, nyumbani na ugenini.

2.Wenye macho wote jana, hivi wameona nini,
Mpira wa danadana, au goli liko ndani,
Hii ni kwa nini mbona, yafanyika ya chooni,
Magoli yawe ya kweli, nyumbani na ugenini.

3.Nani wa kulaumiwa, kwa jambo la uwanjani,
Wale tunawaelewa, walokaa ofisini,
Au ni huyu mwelewa, refa pale uwanjani,
Magoli yawe ya kweli, nyumbani na ugenini.

4.Tunapolia Afrika, turudi pia nyumbani,
Mbeleko timu bebeka, nazo zifike mwishoni,
VARi tukizisimika, ziwe tunazoamini,
Magoli yawe ya kweli, nyumbani na ugenini.

5.Huo ndio ukatili, twauona uwanjani,
Mashabiki ni batili, ya wengine hawaoni,
Wala siyo mabahili, ushindi mwingi wa soni,
Magoli yawe ya kweli, nyumbani na ugenini.

6.Ingekuwa kwingineko, wangerudi uwanjani,
Na marudio yaweko, kweli uwe uwanjani,
Ushindi bila mashiko, si mtamu sikioni,
Magoli yawe ya kweli, nyumbani na ugenini.

7.Kingine kwa timu zetu, magoli mengi fungeni,
Hapo na figisu kwetu, wala ndani hazioni,
Goli moja siyo kitu, ona refa halioni,
Magoli yawe ya kweli, nyumbani na ugenini.

8.Kwenye timu hizi zetu, shida kulenga golini,
Na hasa nyumbani kwetu, kiwango likuwa chini,
Hasa tulishindwa kwetu, kisha jela ugenini,
Magoli yawe ya kweli, nyumbani na ugenini.

9.Pongezi nyingi kwa Yanga, mambo yenu mchezoni,
Hiyo nusu kutotinga, wala msione soni,
Vizuri mmejijenga, zidi kwenda kileleni,
Magoli yawe ya kweli, nyumbani na ugenini.

10.Simba mlishachemsha, kwenye uwanja nyumbani,
Hivyo mmekamilisha, hebu rudini nyumbani,
Pale mlipochemsha, nimekwishawambieni,
Magoli yawe ya kweli, nyumbani na ugenini.

11.Hii kwetu historia, kuwemo mashindanoni,
Timu mbili Tanzania, robo ya CAF amini,
Maandalizi zidia, tutafika kileleni,
Magoli yawe ya kweli, nyumbani na ugenini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news