Tudumishe utamaduni wa kuombeana dua-Rais Dkt.Samia

ZANZIBAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Waislam kudumisha utaratibu wa kuombeana dua ili kuilinda nchi kutokana na majanga mbalimbali ikiwemo mmong'onyoko wa maadili.
Akizungumza kwa niaba yake katika dua maalum ya kumuombea kiongozi huyo huko Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi "B", Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Hajjat Harous Said Suleiman amesema,hatua hiyo itarejesha maadili mema, yanayoonekana kupotea siku hadi siku.

Amesema,jamii inakumbwa na vitendo viovu ambavyo vimeathiri mfumo wa maisha uliokuwepo awali na kuisisitiza jamii kusimamia malezi kulingana na muongozo wa dini ikiwemo suala zima la mavazi ili kuwalinda na vitendo vya udhalilishaji.
Akizungumzia kuhusiana na sherehe za sikukuu ya Idilfitri, inayofanyika mara baada ya mfungo wa Mwezi mtukufu wa Ramdahan amewaomba waislam kuhakikisha wanatoa misaada kwa wenzao wasiokuwa na uwezo ili nao waweze kuwa na furaha ya siku hiyo.

Dkt. Samia ameeleza kuridhishwa na juhudi zinazofanywa na Jumuiya mama ya wanawake wa kiislam Zanzibar katika kuwaelekeza Wanawake wenzao misingi bora ya maisha na malezi ya watoto wao pamoja na kuendesha dua kwa viongozi kwa maslahi ya Taifa.
Amesema kitendo cha kuwaombea dua viongozi ni kizuri, cha kupongezwa na kupigiwa mfano kwani kufanikiwa kwa viongozi hao ndio kufanikiwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Ni vyema kuwaombea viongozi hawa tuliowachagua kwa mapenzi yetu kwani endapo viongozi hao watatereka, watayumba au kuharibikiwa basi ndio tumeharibikiwa wananchi na taifa lote,”amesema Dkt.Samia.
Baadhi ya wana kamati wa jumuiya mama ya wanawake wa kiislam akiwemo Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Hajjat Abla Sultan na Mratibu wa dua hiyo Zahra Ali Hamad wamesema dua hiyo ni sehemu ya kurejesha shukrani kwa viongozi wa nchi kwa wanavyotekeleza vyema majukumu yao kwa wananchi.

"Ikiwa huna cha kumlipa mtu kwa wema aliyokufanyia basi muombee dua," walisema wanakamati hao.
Dua ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeandaliwa na jumuiya mama ya wanawake wa kiislam Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa, taasisi binafsi na wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news