Waliomdhalilisha Mheshimiwa Dkt.Shukuru Kawambwa mbaroni

PWANI-Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limesema limewatia mbaroni watu wawili kuhusiana na tukio la kudhalilishwa kwa Mbunge wa zamani wa Jimbo la Bagamoyo na Waziri Mstaafu katika Serikali ya Awamu ya Nne, Dkt. Shukuru Kawambwa.Kwa mujibu wa taarifa iliolewa leo Aprili 26, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo imeeleza kuwa,Aprili 25, 2024 katika mitandao mbalimbali ya kijamii ilionekana video fupi ikimuonesha Dkt. Kawambwa akishambuliwa kwa maneno makali na kudhalilishwa kwa kufokewa na kutishiwa kufungwa pingu kama mhalifu hali iliyozua taharuki kwa jamii.

“Ukweli ni kwamba tarehe 24 Aprili, 2024 saa 8 mchana huko Kitopeni, Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Waziri na Mbunge mstaafu Dkt.Shukuru Jumanne Kawambwa na mtu mwingine aitwaye Cathbert Enock Madondola walishambuliwa kwa maneno makali, vitisho, dharau na kutishiwa kufungwa pingu na diwani mstaafu wa Kata ya Kilomo Wilaya ya Bagamoyo, Hassani Mwinyi Usinga (Wembe) akiwa na askari mgambo aitwaye Abdallah Mgeni.

“Chanzo cha tukio hilo ni magari ya mchanga ya mtuhumiwa kuharibu barabara na mashamba ya watu yakipita kwenda kubeba mchanga eneo hilo, hali iliyopelekea wananchi kufunga barabara kwa magogo, ili kuzuia uharibifu huo wa barabara.

“Katika clip iliyokuwa inasambaa mitandaoni iliambatana na maneno yaliyosomeka kuwa ‘‘Shukuru Kawambwa waziri wa miundombinu enzi hizo sasa ni dalali wa viwanja Bagamoyo na muhalifu wa kawaida (common criminal)’’ jambo hili pia litachunguzwa ili kubaini ukweli.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani liliwakamata watuhumiwa hao wawili Hassan Mwinyi Usinga (Wembe) na Abdallah Mgeni na baadae kupewa dhamana kwa mujibu wa sheria na watafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika.

“Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamtaka mtu aliyechukua na kusambaza video hiyo mitandaoni ajisalimishe kituo cha Polisi Bagamoyo mara moja,” imesema taarifa hiyo na kuonya wananchi kutojichukulia sheria mkononi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news