Korea yaahidi makubwa Hospitali ya Taifa Muhimbili

DAR-Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Korea ambao ni Wanachama wa Umoja wa Wabunge Marafiki wa Afrika leo wamekutana na Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH-Upanga na Mloganzila) na kujadiliana namna ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Muhimbili na Serikali hiyo.
Akiongea katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa MNH, Dkt. Ellen Senkoro amesema Muhimbili ingependa iongezewe ujuzi katika kuimarisha huduma za ubingwa bobezi ikiwemo huduma mpya ya upandikizaji ini inayotarajiwa kuanza rasmi mwaka 2025.

Amesema, huduma nyingine ni kuimarishwa kwa huduma za upandikizaji figo, uloto pamoja na huduma za wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum, kuendelea kusomesha au kuleta wataalam watakaowajengea uwezo wataalam wa ndani ili kuendana na mahitaji halisi ya wagonjwa hao.
“Tunaipongeza Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia mashirika yake mbalimbali kama KOICA, KOFIH na EXIM kwa kuendelea kushirikiana na Muhimbili-Upanga na Mloganzila, ushirikiano wao umeendelea kuimarisha huduma zetu na kuzifanya ziwe bora zaidi,” ameongeza Dkt. Senkoro.

Naye Mwenyekiti wa Wabunge hao Mhe. Sul Hoon amesema Muhimbili haina tofauti na Hospitali za Korea kwa namna huduma zinavyotolewa, na kuupongeza uongozi kwa huduma bora na kuongeza kuwa maeneo yote waliyopita wamekuta wataalam wakitoa huduma hatua ambayo imesababisha kusiwe na msongamano katika maeneo ya kutolea huduma.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Rachel Mhavile amesema Muhimbili ndio hospitali kubwa na tegemeo yenye huduma za ubingwa na ubingwa bobezi hivyo itaendelea kutoa huduma zinazilingana na hadhi yake.
Serikali ya Tanzania imekuwa na ushirikiano wa takribani miaka 30 na Korea Kusini ambapo katika ushirikiano huo umewezesha baadhi ya mambo ikiwemo kuwajengea uwezo wataalam wa ndani, kuleta wataalam kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika huduma za ubingwa bobezi ikiwemo upandikizaji wa figo kwa kutumia tundu dogo.
Pia, kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo kwa kutumia matundu ya pua, msaada wa magari ya kubebea wagonjwa, hivi sasa Hospitlai ya Taifa Muhimbili iko katika hatua mbalimbali za upembuzi yakinifu wa kuijenga upya hospitali hii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news