Sitanii alichokifanya Paul Makonda mkoani Arusha acha Mungu amlipe

NA GODFREY NNKO

HIVI karibuni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Paul Makonda amewaapisha vijana wa mkoa huo wenye staili ya kipekee kuanzia mavazi hadi utembeaji na wakati mwingine kutenda kwao.
Ni vijana maarufu kama wadudu ili kuwa watu wema, waadilifu katika kutetea na kulinda usalama katika jiji hilo linalosifika kwa utalii duniani.

Pengine huenda hii ni hatua muhimu na mafanikio makubwa ya awali ya RC Makonda tangu ateuliwe Machi 31, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kuuongoza mkoa huo wenye fursa nyingi za kiuchumi na hekaheka nyingi kutoka kwa vijana.

Wakati akiwaapisha vijana hao Mei 2, 2024 mkoani humo, wengi wetu tulifikiria na kumuona RC Makonda kama mtu aliyechanganyikiwa.

Maswali yalikuwa mengi, inakuwaje Kiongozi huyo anayemuwakilisha Rais ngazi ya mkoa anachangamana na wahalifu hao sugu.

Vijana ambao licha ya uhalifu, kipaumbele chao kilikuwa ni kutumia dawa za kulevya hususani bangi ili kwenda kutekeleza maovu yao, iweje RC Makonda ajishughulishe nao badala ya kuagiza wasakwe popote walipo wawajibishwe?.

Hayo na mengine mengi yalikuwa baadhi ya maswali yetu. Lakini, ukweli ni kwamba majibu ya kwa nini RC Makonda alifanya hivyo, alikuwa nayo yeye mwenyewe.

Sitanii na huenda ndivyo ilivyo, jibu sahihi la Mheshimiwa Paul Makonda kujenga ukaribu na vijana hao ni ili kuwafanya kuwa watu wema.

Wema wa vijana hao, ni muhimu zaidi si tu kwa manufaa ya mkoa, shughuli za kiuchumi hususani utalii bali pia, kwa wazazi ambao kila siku wamekuwa wakibubujikwa na machozi.

Vijana hao maarufu kama wadudu kwa miaka mingi wamekuwa mwiba mchungu kwa wakazi wa Arusha ni kupitia matendo yao ambayo awali yalijumuisha wizi wa mali na ukabaji.

Sitanii, ukitaka kupata ukweli na kumbukumbu kuhusu maumivu yanayosababishwa au yaliyosababishwa na wadudu, fika na hoji ipasavyo wakazi wa Muriet, Unga Limited, Moshono, Kwa Mromboo, Makao Mapya, Burka Kisongo, Sakina na kwingineko.

Ndipo utapata majibu kuwa, wadudu ni kundi hatari kwa maisha na ustawi wa maendeleo ya jamii, mkoa na Taifa kwa ujumla.

Katika kumbukumbu zangu, miaka minne iliyopita nilikuwa Arusha Mjini kwa majukumu yangu, baada ya kutekeleza majukumu yangu majira ya saa mbili usiku niliona hakuna umuhimu wa kupanda gari hadi nilipofikia.

Hivyo, niliona nifanye zoezi la kutembelea kwa miguu, lakini ndani ya dakika 10 kabla ya kufika nilipofikia, nilizingirwa na kundi la vijana watatu, vijana hao ambao walikuwa wamebeba silaha za jadi walikuwa wanashinikiza niwape simu na fedha.

Mungu saidia, nilifanikiwa kujihami nikajiokoa katika mikono ya hao wadudu hatari, bila kuniathiri na bila wao kuchukua chochote kutoka kwangu.

Tukio ambalo lina mfanano na hilo, ni mapema Februari mwaka huu nikiwa katika majukumu yangu, majira ya saa moja jioni katikati ya Jiji la Arusha nilishuhudia tukio moja la dada ambaye aliporwa mkoba na wadudu.

Lilikuwa, tukio la huzuni kubwa, kwa sababu aliyeporwa mkoba mle ndani kulikuwa na kompyuta mpakato, fedha na simu.

Jitihada za kuwasaka wale wadudu ambao wanafahamu kila kona ya kupitia na kutokomea kusikojulikana hazikuzaa matunda.

Hivyo, jitihada zinazofanywa na RC Makonda kuwaleta pamoja vijana (wadudu) hao ninaamini zinakwenda kurejesha hadhi ya Jiji la Arusha kuendelea kuwa Geneva of Africa kama alivyowahi kusema Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton.

Itakumbukwa, Bill Clinton mwaka 2000 alipofika Arusha kushiriki mkutano wa kusaka amani ya Burundi alibaini uzuri wa jiji hilo muhimu kwa Afrika na Tanzania, hivyo kutamka kuwa Arusha ni Geneva of Africa.

Arusha kupewa heshima ya kuwa Geneva ya Afrika haikuwa kwa bahati mbaya au kwa upendeleo bali ni kutokana na uzuri na fursa nyingi zilizopo kuanzia shughuli za kitalii, madini, kilimo, ufungaji na nyinginezo nyingi. Na ni makao makuu ya taasisi mbalimbali za Kimataifa.

Kwa hiyo, Arusha ni jiji lenye utajiri, ndiyo maana lina mfanano na Geneva ambalo ni jiji lenye utajiri mkubwa nchini Uswisi.

Pia, ni makao makuu ya benki kubwa za binafsi, taasisi za Umoja wa Mataifa na majumba ya mnada ya Sotheby na Christie, ambayo mara kwa mara huuza mawe ya thamani kwa bei ghali zaidi duniani.

Na Geneva ndiyo jiji ambalo linasifika kwa kulipa mishahara mikubwa wafanyakazi huku amani na utulivu ikitawala.

Mheshimiwa Paul Makonda,sitanii ni ukweli kwamba juhudi zako za kuunganisha vijana hao ambao wamelipa Jiji la Arusha doa kwa muda mrefu ninaamini zinakwenda kuleta matokeo chanya.

Kwanza, ukifanikiwa kuwaunganisha wote wakawa walinzi wa amani wa mkoa na jiji kwa ujumla, tutarajie utulivu ambao utaongeza hamasa ya uwekezaji na kuvutia wafanyabiashara wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Ujio huo, unakwenda kufungua fursa nyingi za kiuchumi na ajira ambazo vijana hao watanufaika nazo kwa namna moja au nyingine. 

Pia, pato la jamii, mkoa na Taifa litaongezeka na huenda Arusha ikaanza kulipa mishahara mikubwa ya Wafanyakazi kama ilivyo Geneva. 

Hilo ni suala la muda na mipango thabiti tu, na inaweza tena kwa asilimia 100.

Pili, tutarajie ongezeko la watalii. Sitanii, hakuna mtalii ambaye anapenda kupata huduma na kupumzika mahali penye uhalifu, kila mmoja anataka utulivu wa nafsi, mali na maisha yake kwa ujumla.

Hivyo, utulivu na amani ya Arusha ni fursa nyine ya kupanua soko kubwa la watalii kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Vile vile, Mheshimiwa Makonda wakati ukiendelea kuwaunganisha vijana (wadudu) hao, endelea kuwaunganisha na fursa za ajira ikiwemo kujiajiri wenyewe ili waweze kuendesha maisha yao.

Ni imani yangu baada ya siku zijazo, huo utamaduni au tabia ya kujiita wadudu na kuvaa vitu vya ovyo ovyo utaondoka ila kwa ninyi kama mkoa kuendelea kuwajenga taratibu taratibu kisaikolojia ili waweze kuondokana na hayo mambo yasiyofaa kwa tamaduni za Kitanzania.

Kumbuka, hakuna mzazi anayezaa mdudu au wadudu bali ni tabia za makundi rika ndizo zinazowapa kiburi cha kujipandikiza majina ya ovyo.

Niendelee kukupongeza Mheshimiwa Paul Makonda kwa ubunifu wako,hakika nimebaini kuwa, ukitaka kushinda vita si lazima utumie silaha kali za moto, bali hata maneno ya hekima na busara yanaweza kumrudisha nyuma adui.

Ikiwa Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa ambayo inafanya vizuri katika Sekta ya Fedha nchini, ninaamini pia vijana hao baada ya kushirikishwa fursa na kuweza kuzitumia kikamilifu wataweza kujitegemea na kuachana na mawazo ya uhalifu.

Rejea,kwa mujibu wa utafiti wa Finscope wa mwaka 2023, utafiti unaonesha, hali ya upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha Arusha uliongezeka na kufikia asilimia 82.2 mwaka 2023, kutoka asilimia 74 mwaka 2017.

Aidha,upatikanaji na utumiaji wa huduma kifedha kupitia benki, uliongezeka na kufikia asilimia 34 kutoka asilimia 29 katika kipindi hicho.

Hivyo, vijana waendelee kushirikishwa fursa kutoka sekta ya fedha ili waweze kuboresha vipato ikiwemo kuboresha maisha yao Arusha.

Sitanii, tunawahitaji kina Makonda wengi wenye upeo wa kuweza kuivusha jamii yetu katika changamoto mbalimbali hususani vijana ambao wanajitumbukiza katika vitendo vy uhalifu kwa kuiga wenzao ili wawe sehemu ya nguvu kazi ya uzalishaji katika Taifa.

Mheshimiwa Makonda, pia usisahau kushirikiana na vijana hao ili muweze kudhibiti uzalishaji na matumizi ya dawa za kulevya jijini Arusha. 

Sitanii, alichokifanya Paul Makonda mkoani Arusha acha Mungu amlipe, wengi wana maumivu yanayotokana na matendo maovu ya wadudu.

Mwandishi wa makala haya ni Mhariri Mkuu wa DIRAMAKINI anapatikana kupitia simu 0719254464.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

4 Comments

  1. Hawa hawafai ESO wamemaliza watu jmn alafu usiku wanatumia mijiwe mukubwa wanavunja milango wanaingia na mapanga mi bisu mnalazwa chin wanachukua kila kitu yaan hawai hao

    ReplyDelete
  2. Mm mwenyew ni mhanga wa hilo walinipora simu😃😃😃😃wako na pikipik. Tena ndo nlitoka kununua nawa naongea na ndugu jamaa na marafiki nkajikuta imepokonywa sikion nlifukuza mpaka miguu ikapelea😃😃😃 watu badala ya kunsaidia wakanambia karibu arusha 🙆‍♀️🙈🙈🙆‍♀️

    ReplyDelete
  3. Watu wa arusha mmepata jembe litumieni vizuli sana mungu ampe maisha marefu

    ReplyDelete
  4. WADUDU HAWAFANYI SANAA,NI WAHALIFU

    Baada ya Kuandika waraka wa Kupinga kitendo cha jamii Kuwapa BRAND/UMAARUFU WADUDU WA ARUSHA,nimeandamwa na baadhi ya watu na Kudai kuwa nawachonganisha na Serikali/jamii ili wasipate riziki,huu ni Mtazamo unaosikitisha ukiusikia kwa mtu wa rika lako au Mkubwa kwako,kwa wale wanaosema WADUDU nation ni Vijana wanaofanya sanaa watujibu maswali kadhaa...
    1. Wadudu mnaodai wanafanya sanaa,wanafanya sanaa gani? Maigizo,Vichekesho au Designer/wanamitindo wa Mavazi?
    2. Kama ndio wameanza sanaa na bado haijawalipa,wanafanya kazi gani kujipatia kipato?
    3. WADUDU nation wako kila mtaa Arusha, je wote hao wanafanya sanaa ya kuwalipa?
    4. Kama ni sanaa kwanini Mda wote wamelewa au wananuka ganja/ugoro? Au sanaa yao haiendi bila vilevi?
    5. Sanaa gani inawafanya mda wote wanatukana? Au kuvunja kanuni za lugha?
    6. Kinachowafanya Wang'oe vifaa vya Pikipiki ni sanaa au Bangi? Yaani pikipiki imeng'olewa kila kitu imebaki siti na vyuma tu,hiyo ndio sanaa?
    7. Sanaa ndio inawafanya wanawafanya walete Vurugu kwenye Mazishi ya Wapendwa wetu?
    8. Yaaani sanaa ndio inakufanya ununue nguo kwa 15k au 20k alafu uitoboe ibaki chengachenga? hiyo nguo umenunua au umeiba?
    9. Sanaa ndio inawafanya wakwapue watu kwenye pikipiki au haisi? Wakijiiita TATU MZUKA?
    10. Sanaa ndio inawafanya wenetu wasione viatu vyote Sokoni/madukani waende kuchonga tairi za Magari,tena oversize?
    11. Sanaa ndio inawafanya wafute Alama za Barabarani?
    12. Sanaa ndio inawafanya wakimbize Pikipiki kwa madai kila Bei ina mwendo wake? Mwendo wa buku,buku 2,buku 3 n.k hii sanaa au roho ya Mauti?
    13. Sanaa ndio inawafanya wawatukane Viongozi wa dini wakiwaonya kuhusu matendo yao? Yaani kuwaambia Viongozi wa dini kwamba Wawaombe radhi na kuwachinjia mbuzi kuwaondolea wanachoita fezeha ndio sanaa? WADUDU nation ndio wakuombwa radhi na kuchinjiwa mbuzi na Mashekh na Wachungaji? Non sense.
    14. Sanaa ndio inawafanya wenetu wadudu watubetue na beto mtaani?
    15. Kama wanafanya Sanaa huko Vichochoroni usiku wanafanya nini?
    16. Sanaa ndio inawafanya wakati wa maafa waseme wameokota magari? Hii sanaa au bangi?
    17. Sanaa ndio inawafanya wanunue Viatu oversize? Alafu wanasema Kila kiatu kinauzwa na mwendo wake,akitembea kama anasukumwa..hiyo ndio sanaa?
    18. Sanaa gani inavuruga tamaduni,ustarabu na mwenendu wa jamii yetu?
    19. Mnajua WADUDU nation wanadai wao hawawi na wenzi? Wakiulizwa mnajitibuje kihisia wanasema wao wanaeee au wananiaje? Kuniaje ni Kubaka au Ushoga, au ndio aina gani ya Sanaa?
    20. Hivi mnajua hawa wadudu wengi wamekataa shule na wana umri kati ya miaka 12 hadi 19?
    21. Hivi mnajua hawa ndio wazazi na Viongozi kwenye jamii ndani ya miaka 5 mpaka 10 Ijayo?
    22. Kuna Kiongozi au Mzazi ambaye anapenda mwanae afanye hii Sanaa ya WADUDU nation?
    23. Kwa hayo Matendo WADUDU nation ni Wasanii au Wahalifu?
    24. Kama ni Wahalifu wa Imani zeru,tamaduni zetu,Mali zetu, na Maadili ya Jamii? Wanastahili kupewa UMAARUFU "BRAND " au Wanastahili "KUZOMEWA na KUZUIWA KISHERIA"? TUWAVUMILIE WATUHARIBIE KIZAZI CHETU?

    N:B Hii ni Vita ya Kizazi hiki,Vyombo vya Habari,Vyombo vya Ulinzi na Mamlaka ya Nchi Tusaidieni kutengeneza Kizazi chenye Matokeo sio Trending za Kijinga📌📌
    Frank Alex Ameandika tena

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news