Tanzania itapata uzoefu usimamizi Madini Mkakati-Mahimbali

BRUSSELS-Imeelezwa kuwa,Tanzania imepata nafasi ya kubadilishana uzoefu na kujadili masuala muhimu yanayohusu usimamizi wa madini hayo muhimu kwa manufaa ya kiuchumi na maendeleo kwa ujumla kupitia Mkutano wa Kimataifa wa Madini Mkakati, Raw Materials Summit 2024 unaoendelea jijini Brussels nchini Ubelgiji.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali akiwa sehemu ya Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano huo unaofanyika kwa siku tatu kuanzania Mei 14 hadi 16, 2024.

Amesema kuwa, Tanzania kama moja ya nchi chache duniani zenye Mkakati wa Madini, Tanzania inashiriki katika Mkutano huo kwa lengo la kubadilishana uzoefu kuhusu usimamizi wa madini hayo muhimu pamoja na kuzungumzia masuala ya uongezaji thamani (value addition) na mchango wa madini mkakati katika mnyororo wa thamani wa sekta ya uzalishaji.

Mahimbali ameongeza kuwa, Wizara ya Madini imelenga kujenga ushirikiano katika utafiti wa kina wa kijiofizikia na wadau mbalimbali duniani, lengo ambalo linaweza kusaidia katika kuimarisha uchumi wa nchi kupitia rasilimali za madini.
“Sekta ya madini ni urithi wa taifa letu. Sekta hii tunaitunza na tunaikuza kwa manufaa ya Taifa na Ulimwengu kwa ujumla. Wizara ya Madini inakusudia kutengeneza ushirikiano katika utafiti wa kina wa kijiofizikia (High Resolution Airbnorne Geophysical Survey) na wadau mbalimbali duniani,” amesema Mahimbali.

Aidha, Mahimbali ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wadau wote wa madini mkakati waliopo katika Mkutano huo kuzungumza na ujumbe huo wa Tanzania ukiwa mjini Brussels na kwamba upo tayari kuwasikiliza na kuwahudumia.

Msafara huo wa Tanzania unaongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji,Prof. Kitila Mkumbo ambapo pia umeambatana na wawakilishi wa sekta binafsi na sekta ya umma kutoka nchini Tanzania.
Katika siku ya kwanza ya Mkutano huo, Mei 14, 2024, Ujumbe huo ulishiriki mjadala wa masuala ya kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya madini, wakati katika siku ya pili, Mei 15, 2024, wameshiriki na kujadili kuhusu kuongeza thamani ya madini.

Sambamba na jinsi ya kujenga ubia wa kimkakati na wadau kutoka Ulaya na Afrika sambamba na Siku ya mwisho Mei 16, 2024, Ujumbe unatarajiwa kushiriki kongamano kuhusu ushirikiano mpya wa kimkakati kati ya Ulaya na nchi zingine, pamoja na uchunguzi wa masoko mapya na upatikanaji wa malighafi muhimu kutoka Afrika.

Baada ya kumalizika mkutano huo, Ujumbe wa Tanzania unatarajiwa kutembelea Soko kubwa la Almasi duniani, Antwerp World Diamond Centre, na kushiriki kongamano la kibiashara kati ya Tanzania na Ubelgiji siku ya Mei 17 2024.

Ziara hiyo inatarajiwa kutoa fursa ya kupata uelewa mpana kuhusu biashara ya Almasi na kufanya mazungumzo ya kibiashara baina ya Tanzania na Ubelgiji kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news