INEC yawashukuru watu wenye ulemavu kwa ushirikiano michakato ya uchaguzi nchini

NA GODFREY NNKO

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema, inathamini mchango wa watu wenye ulemavu katika ushirikiano wao wa mara kwa mara hususani wakati wa michakato ya uchaguzi nchini.
Hayo yamesemwa leo Juni 11, 2024 katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mheshimiwa Mwanaisha Kwariko wakati akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa tume, Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele.
Ni katika mkutano wa tume na wawakilishi wa watu wenye ulemavu nchini ambao umeangazia kuhusu maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini.

"Tume inathamini sana mchango wenu,kwa kuwa ni sehemu ya mafanikio ya kile tulichokusudia kuwaeleza leo.
"Pia, tunawashukuru wawaklishi wa watu wenye ulemavu kwa jinsi ambavyo mmekuwa mkitupa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya tume hasa katika michakato ya uchaguzi.

"Tume inatarajia kupata ushirikiano mkubwa zaidi kutoka kwenu, kwa kuwafikishia wananchi taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu zoezi lililopo mbele yetu la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuwahamasisha wananchi kujiandikisha kuwa wapiga kura."
Jaji Kwariko amesema, katika maboresho hayo ya daftari,tume imewapa kipaumbele maalumu watu wenye ulemavu ili waweze kushiriki kikamilifu kufanya maboresho ya taarifa zao na kujiandikisha.

"Kwa hiyo, tume imekuwa na utaratibu wa mara kwa mara wa kuwashirikisha wadau mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake, kikao hiki ni mwendelezo wa ushirikiano huo."
Julai Mosi, mwaka huu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa anatarajiwa kulizindua rasmi zoezi la maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Kigoma.

Mbali na mambo mengine,maboresho hayo yataiwezesha tume kuwaondoa watu waliopoteza sifa ya kuandikishwa katika daftari hilo na hawana sifa za kupiga kura.
Wasiokuwa na sifa ni iwapo mtu yupo chini ya kiapo cha nchi nyingine,hana akili timamu, lakini lazima ithibitike kwa mujibu wa sheria.

Aliyewekwa kizuizini kama mhalifu, ulemavu wa akili, kutiwa hatiani kwa kosa ambalo adhabu yake ni kifo au mtu anayetumikia adhabu zaidi ya miezi sita jela.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news