Waziri Simbachawene aitaka TAKUKURU kuja na mwarobini wa migogoro ya ardhi nchini

NA LUSUNGU HELELA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutupia jicho sekta ya ardhi inayoonekana kushamiri migogoro ya ardhi inayotishia ustawi wa wananchi na jamii kwa ujumla.Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri Mhe. George Simbachawene wakati akifungua mafunzo ya awali ya uchunguzi mwaka 2024, kwa maofisa wa TAKUKURU katika Shule ya Polisi Tanzania iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mhe. Simbachawene amesema maeneo ya kutolea huduma nchini bado ni tatizo na sekta ambayo imeumiza nchi na kuleta migogoro mikubwa kwa familia na jamii ni sekta ya ardhi, hivyo kuitaka taasisi hiyo kuitupia jicho kwa karibu na kuja na suluhisho.

Amesema, kuna haja ya TAKUKURU kufanya utafiti katika sekta ya ardhi, kubaini chanzo cha migogoro hiyo na kuja na mapendekezo ambayo yataisaidia Serikali kukabiliana na migogoro hiyo.

‘‘Msisitizo wangu, Mkurugenzi wa TAKUKURU ikite zaidi maeneo ya kutolea huduma kwani kuna tatizo kubwa...wapo wenzetu wengine kwa kweli wanageuza sehemu za kutoa huduma kama ndiyo sehemu yao ya kupata kiinua mgongo na utajiri.
"Na sekta ambayo imeiumiza nchi hii sana na imeleta migogoro mikubwa sana, kusumbua familia na jamii ni sekta ya ardhi.

"Kila mkoa, kila mahala kuna mgogoro wa ardhi, inadumaza maendeleo na inaharibu malengo ya baadhi ya watu.Unampa kiwanja huyu, halafu unashangaa mtu mwingine amepewa, unakuta hati zinagongana mbili.

"Hivi tunashindwaje kuwatafuta hao wote waliohusika popote walipo waje wajibu?.‘'TAKUKURU tusaidieni kwenye hili, kwa sababu migogoro ya ardhi inatengenezwa, halafu watu wanalakamika na viongozi wakipita wanaanza kusuluhisha migogoro na ni kwa sababu ya watu ambao tulikuwa tunawachekeachekea.’’

Pia, ameitaka TAKUKURU kushirikiana na vyombo vingine, ikiwemo polisi na Tume ya Maadili kushughulika na wale wanaoghushi nyaraka za ardhi na kujipatia hati miliki kinyume cha sheria.

"Sasa hivi katika maeneo mengi watu wanalalamika, Waziri wa Ardhi anahangaika huko na huku, watu wamegushi nyaraka. Kugushi ni jinai, TAKUKURU shirikianeni na vyombo, ikiwemo Jeshi la Polisi na Tume ya Maadili, muweke mkakati wa pamoja wa kushughulika na hii sekta ya ardhi,"amesema.

Awali, akitoa taarifa, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Cp. Salum Hamduni amesema maofisa uchunguzi wanaopatiwa mafunzo ya awali ya uchunguzi ni 310, wachunguzi wasaidizi 110 na watumushi 16 wanabadilisha kada.Amesema,washiriki hao waliwasili shuleni hapo Mei 31,2024 tayari kwa mafunzo ya awali ya uchunguzi ambayo yatafanyika kwa miezi mitano na kwamba ni ya muhimu na lazima kwa maofisa uchunguzi wote wa TAKUKURU.

Kuanzia mwaka 2022, Serikali imeipatia TAKUKURU vibali vya kuajiri watumishi 1,190 ambapo mwaka 2021/2022 tulipata kibali cha kuajiri watumishi 450 ambapo waajiriwa wapya ni 380 na ajira mbadala 70.

"Mwaka 2022/2023 tulipata kibali cha kuajiri watumishi 320,waajiriwa wapya 250 na ajira mbadala 70 na mwaka 2023/2024 tumepata kibali cha kuajiri watumishi 420 ambapo waajiriwa wapya ni 350 na ajira mbadala ni 70,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news