DODOMA-Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara ya Madini na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia Sheria Ndogo za Halmashauri ili kuondoa changamoto wanazokumbana nazo Wachimbaji Wadogo wa Madini.

Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza, Wizara ya Madini na TAMISEMI kupitia sheria ndogo za Halmashauri zinazowaletea changamoto wachimbaji wa madini ili kufanya marekebisho yatakayowawezesha wachimbaji kuendelea kuchimba kwa amani na tija zaidi na hatimaye kuongeza mchango wao katika maendeleo ya Sekta ya Madini.




Pia, amewahimiza wachimbaji wa madini kuendelea kutumia Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri, maono ambayo kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Wizara imepanga kufanya utafiti wa kina (High-Resolution Airborne Geophysical Survey) wa miamba yote yenye madini iliyopo hapa nchini, ili kupata taarifa za uhakika za aina ya madini yaliyopo nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema Wizara inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuongeza tija katika sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuwapa wachimbaji wadogo maeneo ya kuchimba na kuwapatia leseni ili wafanye uchimbaji bila usumbufu sambamba na kufuta leseni zote zisizofanyiwa kazi au kuendelezwa, na kuondoa maombi mengi ya leseni ili kutoa nafasi kwa watanzania kuchimba madini kwa tija.
Ameongeza kuwa, Wizara imeanzisha programu maalum ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) kwa ajili ya kusaidia vijana na wanawake kwa kuwapatia maeneo ya kuchimba pamoja na vifaa ili waweze kujiajiri na kufanya kazi ya uchimbaji kwa ufanisi na tija zaidi.



Vilevile, ameiomba Serikali kuendelea kununua mitambo ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kuhakikisha inayafikia maeneo yote kwa usawa.
