DAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na Waziri wa Uchumi na Maendeleo wa Shirikisho la Urusi, Bw. Maxim Reshetnikov na kujadiliana naye masuala mbalimbali yakiwemo yanayogusa biashara, kilimo, usafirishaji, elimu, nishati na utalii.


Akielezea kuhusu fursa zilizopo nchini, Waziri Mkuu amesema Tanzania inapakana na bahari yenye bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga. “Ina maziwa ya Victoria, Tanganyika, Nyasa na yenye bandari kadhaa. Ziwa Victoria kuna bandari kule Kagera, Mwanza na Musoma. Ziwa Tanganyika kuna bandari za Kigoma, Kabwe na Kasanga na Ziwa Nyasa kuna bandari za Mbambabay na Kyela.”

Amesema, bandari hizo zimeunganishwa na barabara, reli ya kati, TAZARA, reli ya SGR na vyote vinaenda hadi nje ya nchi ili kurahisihwa usafirishaji wa bidhaa. “Tunao usafiri wa uhakika kutoka Dar es Salaam hadi Kapiri-Mposhi, Zambia ambako bidhaa zinachukuliwa na kupelekwa nchi nyingine. Pia SGR itakapokamilika, itawezesha kufikisha mizigo hadi Rwanda, Uganda na Congo.”
Kuhusu kilimo, Waziri Mkuu amewakaribisha wafanyabiashara kutoka Urusi waje kuwekeza kwenye kilimo kwa kuwa Tanzania ina eneo kubwa la ardhi na lenye rutuba kwa ajili ya shughuli za uzalishaji. “Malengo ya Tanzania ni kuona tunakuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula barani Afrika.”

“Tanzania ni lango kwa nchi nane zinazotuzunguka na mbili ziko mbioni kujiunga. Nchi hizo ni Kenya, Uganda, DRC, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na Msumbiji. Kuna nchi mbili za Comoro na Sudan Kusini ambazo nazo zimeonesha nia na pia Somalia tunaendelea na mazungumzo."


Kwa upande wa elimu, Waziri huyo alisema nchi yake itaendelea kuisaidia Watanzania kunufaika na fursa za masomo nchini Urusi kutokana na bajeti ya Serikali. “Hivi sasa kuna nafasi 90 za wanafunzi wa Kitanzania kusomea vyuo vikuu vya Urusi kuanzia mwaka ujao. Tuko tayari kuongeza idadi hiyo endapo itabidi,” alisema Waziri Reshetnikov.