DAR-Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema kuwa uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China umeendelea kukua ambapo mwaka 2023 biashara kati ya nchi hizo ilifikia dola bilioni 8.78.
Amesema kuwa ukuaji na ushirikiano huo wa makampuni ya China na wafanyabiashara wa Tanzania umeleta maendeleo katika ukuaji wa viwanda vya ndani, kutengeneza ajira, ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa hali ya maisha ya Watanzania.
Amesema hayo leo Novemba 30, 2024 wakati wa hafla ya Kumbukumbu ya Miaka Kumi ya Jumuiya ya Kukuza Ushirikiano kati ya China na Tanzania, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Dar ea Salaam, jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa, Kampuni za China zimezindua takribani miradi 1,274 ambayo kwa kiasi kikubwa pamoja na mambo mengine, imezalisha ajira kwa Watanzania.
“Huu ni uthibitisho wa jinsi ushirikiano wetu unavyolenga kutoa fursa kwa wananchi wetu.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anathamini mchango wa China katika maendeleo ya Tanzania kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za biashara, miundombinu na utamaduni.”
Aidha, amesema kuwa China ni moja ya mshirika mkubwa wa kibiashara na uwekezaji kwa Tanzania na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo kwenye sekta za kilimo, madini, viwanda na maendeleo ya miundombinu.
Ameongeza kuwa China imekuwa mshirika muhimu katika kuisaidia Tanzania kukabiliana na majanga ya kiafya ikiwemo magonjwa ya kuambukiza na changamoto za afya ya mama na mtoto.
“China imekuwa ikitoa timu za wataalam, kuchangia vifaa, na kusaidia kujenga miundombinu ya afya. Ushirikiano huu umeokoa maisha ya wengi na umehakikisha kwamba watu wetu wanapata huduma bora za matibabu.”