DAR-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Sera za Uchumi na Fedha), Dkt. Yamungu Kayandabila, amekutana na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Jesper Kammersgaard, aliyeambatana na Makamu wa Rais wa Mfuko wa Uwekezaji wa Serikali ya Denmark (IFU), Bw. Theo Larsen.
Katika mkutano huo uliofanyika katika ofisi za BoT jijini Dar es Salaam, pande zote zilijadili fursa zilizopo za ubia kati ya Tanzania na Denmark za mikopo ya masharti nafuu na dhamana kwa ajili ya uwekezaji.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Kayandabila ameueleza ujumbe huo kuwa Benki Kuu kama wakala wa Serikali husimamia Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa ajili ya Mauzo Nje ya Nchi (Export Credit Guarantee Scheme-ECGS) na Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (Small and Medium Enterprises Guarantee Scheme-SME-CGS) ambayo inalenga kuondoa changamoto ya sharti la dhamana linalotolewa na benki nchini ili kutoa mikopo kwa wahitaji.






