Kupanga ni kuchagua

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kwamba, kila binadamu ana mamlaka ya kubadilisha maisha yake kwa kutumia mazingira aliyo nayo ili kuwa kile anachokitaka.
Wahenga wakasema kuwa,mipango mibovu ya maisha husababisha maisha kuwa mabovu na mipango bora ya maisha husababisha maisha kuwa bora zaidi.

Kupanga mambo kwa ufanisi ni sawa na kufanya maamuzi ya busara. Kila wakati tunapokuwa na machaguo mengi, tunahitaji kuchagua yale muhimu na yanayofaa ili kufikia malengo yetu.

Hii inaonesha umuhimu wa kuchagua kwa makini na kuwa na mpango ili kuepuka kuchanganyikiwa na kufikia mafanikio.

Chambuzi nyingi za wataalamu katika maeneo ya usimamizi, uongozi na saikolojia zimeainisha dhana ya kupanga ni kuchagua kama sehemu muhimu ya mchakato wa maamuzi yeye tija.

Mfano katika uongozi na usimamizi, wataalamu wanaona kupanga kama hatua muhimu ya kufanya maamuzi kwa ufanisi.

Aidha,kutokana na wingi wa rasilimali, muda, na fursa zinazopatikana,wahusika wanatakiwa wachague vipaumbele vya kutumia rasilimali hizo kwa ufanisi.

Hii inamaanisha kwamba, kupanga ni mchakato wa kuchagua malengo, mikakati na hatua zinazokubaliana na vipaumbele vya mtu, asasi,ofisi au mamlaka fulani.

Kwa upande wa wataalamu wa saikolojia wanaona kwamba, kila wakati tunapokuwa na machaguo mengi, tunahitaji kuchuja na kuchagua lile linalofaa zaidi kwa hali yetu.

Aidha,hii inaweza kuwa na athari kubwa kwa ufanisi wetu, kwani kuchagua kwa busara huleta ustawi na kurahisisha mchakato wa kufanya maamuzi.

Ni kwa mantiki hiyo, mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, kupanga ni kuchagua ili kuyafikia malengo yako.Endelea;

1. Kama washindwa kupanga, jua wapanga kufeli,
Walieleza wahenga, maneno haya ni kweli,
Tukumbushane kulonga, tusijeanguka chali,
Kupanga ni kuchagua, kuyafikia malengo.

2. Kwenda bila ya kupanga, umeharibu shughuli,
Badala kwenda Upanga, kula pilau na wali,
Utajikuta watinga, sipitali Muhimbili,
Kupanga ni kuchagua, kuyafikia malengo.

3. Ni wale wanaopanga, waweza pima umbali,
Kama mbele wanasonga, au wanadiledali,
Kwamba yao wanajenga, au ni dhofulihali,
Kupanga ni kuchagua, kuyafikia malengo.

4. Vema sana kujipanga, hatua zile za kweli,
Uendako unalenga, hata kama kuko mbali,
Kwa wakati utatinga, kwa haki pia adili,
Kupanga ni kuchagua, kuyafikia malengo.

5. Kazi bila daftari, ni maisha ya tumbili,
Kwamba kwake iwe hari, anavyokula hajali,
Kwa wanadamu hatari, sababu tuna akili,
Kupanga ni kuchagua, kuyafikia malengo.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news