Naibu Gavana Sauda Msemo aongoza mbio maalum Miaka 80 ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Ashira

KILIMANJARO-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania anayeshughulikia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, ameongoza mbio maalum tarehe 22 Machi 2025 ya kuadhimisha miaka 80 ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Ashira, iliyopo mkoani Kilimanjaro.
Mbio hizo zilifuatiwa na mahafali ya 33 ya wanafunzi wa kidato cha sita, ambapo Naibu Gavana Msemo alikuwa mgeni rasmi. Katika hotuba yake, alitoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kujenga vyumba tisa vya madarasa, hatua ambayo imeimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia shuleni hapo.
Aidha, aliwahimiza walimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuboresha viwango vya ufaulu wa wanafunzi. Kwa upande wa wanafunzi, aliwataka kujituma katika masomo yao kwa lengo la kuweka rekodi ya wahitimu wote 439 kufaulu kwa daraja la kwanza.
Naibu Gavana Msemo ni mmoja wa wahitimu wa shule hiyo miaka 34 iliyopita ambapo kwa kushirikiana na wahitimu wenzake wametoa msaada wa meza 254, viti 254, vitanda 8, pamoja na kufanikisha ujenzi wa tanuri la kuchomea taka na mchango wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa chombo cha usafiri kwa shule hiyo.
Akitoa shukrani kwa mgeni rasmi, Mkuu wa Shule, Bi. Zainabu Sheshui, amesema kuwa misaada hiyo itawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora, huku walimu wakitekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi ili kuinua kiwango cha elimu shuleni hapo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news