MBEYA-Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimezindua operesheni yake ya ‘No Reforms, No Election’ katika Kanda ya Nyasa mkoani Mbeya, lakini uzinduzi huo umeshindwa kuwavuta wananchi kwa wingi kama walivyotarajia.
Badala yake, wananchi wameonyesha wazi kwamba hawana imani na ajenda yao ya kugomea uchaguzi kwa kisingizio cha mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi.
Katika viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya, ambapo uzinduzi huu ulifanyika Machi 23, 2025 idadi ndogo ya wananchi waliojitokeza ilidhihirisha wazi kwamba CHADEMA imepoteza mvuto wa kisiasa na haina tena uungwaji mkono wa wananchi kama ilivyokuwa ikidai.
Pamoja na jitihada za Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, kuhamasisha wafuasi wake, wengi wao hawakuonekana kujali.
Taarifa zinaeleza kuwa,hata ziara za viongozi wa chama hicho katika maeneo mengine ya Kanda ya Nyasa hazijapata mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi.
Kwa mfano, ziara ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, katika wilaya za Kyela, Busokelo, na Rungwe, imeonekana kusuasua huku wananchi wakikwepa kushiriki mikutano hiyo.
Katika mahojiano na baadhi ya wananchi, wengi walieleza kuwa, wanatambua juhudi zinazofanywa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha mazingira ya uchaguzi na kuwa CHADEMA wanatumia propaganda za kugomea uchaguzi kama kisingizio cha kuhalalisha kushindwa kwao kwenye uchaguzi ujao.
“Hakuna chama cha siasa kinachoshinda kwa kukwepa uchaguzi, wananchi wanataka maendeleo, siyo maandamano na migomo isiyo na tija,” alisema mmoja wa wananchi waliokuwepo eneo la tukio.
Hali hii inaendelea kuthibitisha kuwa ajenda ya ‘No Reforms, No Election’ ni propaganda isiyowagusa Watanzania wengi, ambao wanapendelea kushiriki kikamilifu katika michakato ya kidemokrasia badala ya kususia uchaguzi kwa sababu zisizo na msingi.
Kwa mara nyingine tena, CHADEMA wameonyeshwa mlango na wananchi, ambao sasa wanataka siasa za maendeleo na siyo siasa za vurugu na malalamiko yasiyo na mwisho.
Tags
Habari
