DAR-Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kinasikitika na kulaani vikali tukio la kushambuliwa, kudhalilishwa, na kudhuriwa kwa msichana mmoja (jina lake bado halijatambulika) linalosambaa kwenye mitandao ya kijamii kupitia picha mjongeo, linalodaiwa kuwa wahusika ni wanafunzi.
Tayari, Chuo kinafatilia taarifa za tukio hilo kwa kiini ili kubaini uhalisia wake; na utambulisho wa wahusika.
Endapo itabainika kuwa wahusika ni wanafunzi wa UDSM, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria, taratibu, kanuni na miongozo ya UDSM.
Aidha, Chuo kitashirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha kuwa Sheria za nchi zinazingatiwa.
UDSM inapinga aina yoyote ya ukatili, udhalilishaji au uvunjaji wa haki za kibinadamu ndani na nje ya mazingira ya Chuo. Pia, UDSM itasimama imara kulinda utu, usalama, na hadhi ya kila mwanafunzi na wanajumuiya wengine wa Chuo bila upendeleo.
Kwa mantiki hiyo, Chuo kinatoa rai kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla kuzingatia Sheria, kanuni, taratibu, na miongozo ya chuo; na maadili ya Kitanzania.