NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema katika kipindi cha mwezi Machi na Aprili, 2025 kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola imefanikiwa kuzuia tani 14 za kemikali bashirifu zilizokuwa ziingizwe nchini kinyume cha sheria nchini.

Kamishna Jenerali wa DCEA,Aretas Lyimo ameyasema hayo leo Aprili 24,2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema, pia katika operesheni hiyo walifanikiwa kuteketeza ekari 178 za mashamba ya bangi pamoja na kushikilia magari saba, pikipiki tano na bajaji moja vilivyohusika kwenye uhalifu huo.
Lyimo amesema, operesheni hiyo imefanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Shinyanga, Tabora, Tanga, Songwe, Mbeya na Arusha.
"Jumla ya watuhumiwa 35 wamekatwa na taratibu za kisheria zinaendelea dhidi yao."
Kamishna Jenerali Lyimo amesema, mamlaka kwa kushirikiana na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Duniani (INCB) na mamlaka nyingine za udhibiti ilibaini na kuzuia kilogramu 4,000 za kemikali aina ya 1-Boc-4-piperidone.
Sambamba na kilogramu 10,000 za kemikali aina ya Acetic anhydride zilizokuwa ziingizwe nchini kutokea barani Asia bila kuwa na vielelezo vinavyoonesha matumizi ya kemikali hizo.
"Endapo kemikali hizi zingeingizwa nchini na kuchepushwa zingeweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya aina ya fentanyl na heroin.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema,matumizi ya kiasi hicho cha dawa za fentanyl ambazo zingezalishwa zingeweza kusababisha vifo kwa watumiaji bilioni nne ikizingatiwa kwamba kilogramu moja ya dawa hizo inaweza kusababisha vifo kwa watu 500,000 kutegemea na uzito,afya, na historia ya mtumiaji.
Amesema,miligramu mbili inaweza kusababisha kifo kwa mtu mmoja. "Kemikali aina ya acetic anhydride inaweza kutumika katika mchakato wa kutengeneza dawa za kulevya aina ya heroin.
"Hivyo, kiasi cha kilogramu 10,000 kilichozuiliwa kingeweza kutumika kutengeneza kilogramu 3,704 za heroin."
Aidha, amesema kemikali hiyo inaweza kutumika kuzalisha kemikali nyingine bashirifu ambazo zinaweza kutumika kuzalisha dawa za kulevya za mandrax na methamphetamine.
Kamisha Jenerali Lyimo amesema,uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa unaendelea ili kubaini mitandao zaidi ya usafirishaji haramu wa kemikali bashirifu zinazoweza kuchepushwa na kutengeneza dawa za kulevya.
Wakati huo huo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema,katika operesheni zilizofanyika mkoani Mbeya, raia wa Uganda Herbert Kawalya mwenye hati ya kusafiria Na. B00132399 na mmiliki wa kampuni ya Hoxx Wells Lux Tour Limo, alikamatwa akiwa na pakti 10 za pipi zenye uzito wa gramu 174.77.
Ni zilizotengenezwa kwa dawa za kulevya aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu ya tetrahydrocannabinol (THC).
"Ukamataji huo, ulikwenda sambamba na ukamataji wa gari ndogo aina ya Mercedes Benz yenye namba za usajili MG 33 BM GP iliyokuwa inasafirisha pipi hizo kuingia nchini kutokea Afrika Kusini.
"Utengeneza wa pipi hizi zenye kiwango kikubwa cha sumu aina ya THC ni ushahidi wa nia ovu ya wahalifu kulenga kuharibu vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa."
Aidha, katika tukio lingine mkoani Mbeya,Kamishna Jenerali Lyimo amesema, zilikamatwa kilogramu 1,658 za bangi aina ya skanka na kilogramu 128.7 za bangi zilizokuwa zinaingizwa nchini kutoka nchini Malawi.
"Operesheni zilizofanyika jijini Dar es Salaam, zilifanikisha ukamataji wa kilogramu 220.67 za bangi aina ya skanka katika Kata ya Chanika zikiwa zimefichwa chooni huku kilogramu 11 zikikamatwa eneo la ukaguzi wa mizigo kwenye bandari ya kuelekea Zanzibar."
Katika operesheni zilizofanyika mikoa ya Arusha, Tanga, na Manyara ameswma zilikamatwa kilogramu 733.74 za dawa ya kulevya aina ya methamphetamine, kilogramu 91.62 za heroin, kilogramu 692.84 za mirungi iliyokuwa inaingizwa kutokea nchini Kenya na kilogramu 115.05 za bangi pamoja na kuteketeza ekari mbili za mashamba ya bangi.
Vilevile, operesheni zilizofanyika katika Wilaya ya Uyui na Nzega mkoani Tabora amesema, kilogramu 845 za bangi zilikamatwa na ekari 176 za mashamba ya bangi ziliteketezwa.
Kadhalika,kilogramu 98.35 za dawa za kulevya aina ya bangi zilikamatwa katika operesheni zilizofanyika wilayani Kahama na Shinyanga.
Amesema,udhibiti wa dawa za kulevya na kemikali bashirifu uliofanyika, umezuia athari kubwa ambazozingejitokeza kiafya, kijamii, kiuchumi na kimazingira ikiwemo kuongezeka kwa dawa za kulevya mtaani.
Pia,ukamataji huu umesaidia kuokoa nguvu kazi ya Taifa ambayo ingeangamia endapo dawa hizo zingeingizwa mitaani.
"Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inatoa wito kwa wananchi kuendeleza ushirikiano kwa kutoa taarifa mapema wanapohisi au kuona uwepo wa shughuli zinazohusiana na biashara au uzalishaji wa dawa za kulevya katika maeneo yao kupitia kituo chetu cha taarifa na huduma kwa kupiga namba 119 bure.
"Vilevile, wazazi na walezi mnahimizwa kuwa makini na kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wenu ikiwa ni pamoja na kuwaasa wajepushe na mazingira na sababu zozote zinazoweza kuwaingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya.
"Pia, tunazikukumbusha kampuni zinazojihusisha na biashara na matumizi ya kemikali za viwandani na kilimo kuzingatia matakwa ya sheria za nchi na kuepuka kushirikiana na magenge ya kihalifu kusafirisha kemikali bashirifu ambazo zinaweza kuchepushwa na kutengeneza dawa za kulevya."
Tags
Breaking News
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)