Dkt.Nchemba aongoza Ujumbe wa Tanzania mikutano ya Kipupwe ya IMF na Benki ya Dunia jijini Washington D.C

WASHINGTON D.C-Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewasili Washington D.C nchini Marekani, ambako anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mikutano ya Msimu wa Kipupwe ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, ambayo Mwaka huu 2025, imebeba kaulimbiu ya “Ajira: Njia ya Mafanikio”.
Katika msafara huo, Mhe. Dkt. Nchemba ambaye ni Gavana wa Benki ya Dunia, ameambatana na Magavana wasaidizi wa Benki hiyo, ambao ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba.
Viongozi wengine ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban na Viongozi wengine waandamizi wa Serikali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Ujumbe wa Tanzania, umekaribishwa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Dkt. Elsie Kanza na kufuatiwa na kikao cha maandalizi kilichofanyika Ubalozi wa Tanzania mjini Washington D.C ambapo pamoja na mambo mengine, Mhe. Balozi Kanza alitoa taarifa ya utendaji kazi wa Ubalozi huo, iliyoonesha mafanikio makubwa katika kukuza biashara na diplomasia ya kiuchumi kati ya Tanzania na Marekani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news