KATIKA hali inayozua maswali mengi, taarifa zimeibuka zikidai kuwa shilingi milioni 24 zilizochangwa na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) kwa ajili ya kusafirisha watu kutoka mikoani kuja Dar es Salaam kushiriki maandamano na vurugu siku ya kesi ya Mwenyekiti wa Chadema,Tundu Lissu, zimetafunwa na wajanja wachache.
Kwa mujibu wa vyanzo vya karibu na mpango huo, michango hiyo ilikusanywa kwa lengo la kugharamia usafiri, malazi na chakula kwa watu waliotakiwa kusafirishwa kutoka sehemu mbalimbali za nchi kuja Dar es Salaam kuonyesha nguvu ya kuunga mkono harakati na kuishinikiza serikali kupitia maandamano na nguvu ya umma ili kufuta kesi inayomkabili Mwenyekiti Tundu Lissu Mahakamani.
Michango hiyo ilikusanywa na Liberatus Mwang'ombe kwa upande wa Marekani na Albin Saragu kwa upande wa Ulaya ambao wanatajwa kuwa viongozi wa Diaspora wa maeneo hayo.
Michango hiyo ilipatikana na ikakabidhiwa kwa Mwenyekiti wa kamati ndogo ya fedha iliyoundwa na Kamati Kuu kwa kutumwa kwenye akaunti yake binafsi ya Benki ambayo aliwatumia wakusanyaji.
Hata hivyo, hali imeelezwa kuwa tofauti kabisa na matarajio kwani Watu waliotarajiwa kusafirishwa hawakuonekana kuwapo na hasa vijana wa ulinzi ambao walikuwa wameandaliwa ili kuwapa viongozi ulinzi Mahakamani, vilevile wananchi kutoka Mikoa mbalimbali hawakuonekana kwa wingi uliopangwa, huku baadhi ya waliokuwa waandaji wa ndani wakilalamikia ukosefu wa fedha uliosababisha mipango yao kufeli.
Pia zipo hujuma za ndani zilizofanyika baada ya mjumbe mmoja wa mkakati huo kuuvujisha kwa kuandika idadi ya mabasi ambayo yalikuwa yameandaliwa kusafirisha watu kutoka mikoa mbalimbali (Mdude Nyagali alitweet na alitaja kuwa yalikuwa yameandaliwa mabasi 41).
Taarifa za ndani zinadai kuwa sehemu kubwa ya fedha hizo zilitafunwa na zile kidogo zilizopelekwa Mbeya, Musoma na Arusha hazikutumika kabisa na waliokabidhiwa jukumu la kuratibu matumizi, na badala ya kufanikisha malengo yaliyokusudiwa, walijinufaisha binafsi.
"Kulikuwa na matumaini makubwa kwamba watu kutoka mikoa kama Mwanza, Arusha, Mbeya na Mara wangekuwa Dar kwa siku hiyo muhimu,"alisema mmoja wa waandaaji wa shughuli hiyo aliyeomba jina lake lihifadhiwe.
"Lakini wengi wao walikosa nauli na msaada wa malazi; tulibaki na aibu kubwa mbele ya umma kwa kutokuwa na watu wengi siku ya Aprili 24,2025.
Hali hii imeibua mjadala mpana miongoni mwa wanaharakati na wafuasi wa Mh Lissu kuhusu uaminifu wa baadhi ya viongozi wa vuguvugu la mabadiliko, hasa wale walioko nchini. Wapo wanaodai kuwa matukio kama haya yanadhoofisha kwa kiasi kikubwa harakati za kisiasa na huondoa imani ya Watanzania waishio nje kuendelea kuchangia au kushiriki kwa njia ya kifedha katika jitihada za ndani na wanaona kama kuna hujuma kubwa sana zinafanywa dhidi ya Lissu na watu wake wa karibu ambao aliwaamini.
Mpaka sasa, bado hakuna taarifa rasmi kutoka kwa viongozi wa Diaspora (Liberatus Mwang'ombe na Aubin Saragu) waliohusika na ukusanyaji wa fedha hizo wala kutoka kwa timu ya Waratibu wa harakati hizo hapa Tanzania kuhusu sakata hilo.
Hali hii inaacha maswali mengi kuhusu mustakabali wa mshikamano kati ya wafuasi wa Mh Lissu wa ndani na wale wa nje ya nchi.
Tukio hili linaonesha changamoto kubwa inayowakabili wanaharakati walioko ndani ya Chadema kuhusu uaminifu wao kwenye masuala ya fedha.
Kwenye Clubhouse ya jana Jumatatu tarehe 28 Aprili,2025 iliyoendeshwa na Sauti ya Watanzania, wajumbe walihoji japokuwa Liberatus na Saragu hawakuwepo jambo ambalo sio kawaida kwani ilikuwa mahususi kwa ajili ya kufanya tathimini, kikao cha kamati ya uongozi kilichofanyika juzi pia hawakuhudhuria kikao ili waweze kutoa mrejesho wa taarifa ya fedha hasa matumizi yake.
》Tutaendelea kuwajuza yatakayojiri》
Tags
Habari
