WASHINGTON-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, ameshiriki kikao kati ya ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, na Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Adran Ubisse.

Dkt. Nchemba alieleza kuwa Tanzania imejipanga kukabiliana na athari za kusitishwa kwa misaada kutoka Marekani kwa kutegemea rasilimali za ndani kupitia Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Alibainisha kuwa Serikali imejipanga kubana matumizi ya kawaida na kuelekeza fedha zaidi kwenye huduma muhimu za jamii pamoja na sekta za uzalishaji, kwa lengo la kulinda uchumi wa taifa na kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma muhimu bila kutegemea misaada ya nje.
Mazungumzo hayo yamefanyika kando ya Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya IMF na Benki ya Dunia, inayoendelea jijini Washington D.C., Marekani.