NA LWAGA MWAMBANDE
KILA mmoja anatambua kuwa,Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) dhima yake kuu ya sasa na ijayo ni maendeleo na ustawi wa jamii miongoni mwa nchi wanachama.
Licha ya dhima hiyo yenye nia njema kwa wananchi zaidi ya milioni 300, miongoni mwa wanachama wa jumuiya hiyo wameendelea kuwa na ubinafsi ikiwemo makwazo. Mfano ni Malawi na Afrika Kusini ambao ni kati ya mataifa 16 ya SADC.
Ni hivi karibuni, Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe alibainisha kuwa,Serikali imepokea taarifa kuwa Serikali ya Malawi imezuia kuingia kwa mazao ya kilimo kutoka Tanzania, yakiwemo unga, mchele, tangawizi, ndizi, na mahindi.Hatua hiyo imeathiri moja kwa moja shughuli za wafanyabiashara wa Kitanzania wanaosafirisha bidhaa hizo kwenda Malawi.
Waziri amebainisha hayo ikiwa kwa kipindi cha miaka mitano, Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kufungua soko la ndizi nchini Afrika Kusini bila mafanikio.
Hali hii inafanana na changamoto ambazo Tanzania ilizopitia kwa zaidi ya miaka kumi katika kufungua soko la parachichi, hadi pale walipoamua kuchukua hatua za kulinda maslahi ya nchi.
Changamoto za namna hii ni wazi zinalenga kudhoofisha kabisa maono mazuri ya kuelekea Mtangamano wa Kikanda (Regional Integration) ili kupata eneo huru la biashara,umoja wa forodha, soko la pamoja, umoja wa kiuchumi na umoja wa kisiasa.
Kutokana na ubinafsi huo wa Malawi na Afrika Kusini, tayari Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ametangaza uamuzi mgumu dhidi ya nchi hizo kwa kuzuia mazao yoyote ya kilimo kuingia nchini kutokana na nchi hizo kukakataa kubadili msimamo wao wa kuruhusu mazao kutoka Tanzania kuingia kwenye nchi zao.
Waziri Bashe ametangaza uamuzi huo usiku wa Aprili 23, 2025 huku akisema msimamo ni kupiga marufuku matunda kama matufaa (apples)na mengine kutoka Afrika Kusini kuingia nchini hadi watakapoondoa zuio kwa Tanzania.
Ni kutokana na kadhia hii, mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anahoji kama SADC ni wamoja au porojo za hapa na pale.Endelea:
1. Ya kwamba wagombanao, ni hao wapatanao,
Wanayajua ya kwao, watayamaliza wao,
Ndivyo twawaona hao, vita yao ya mazao,
Hivi SADC wamoja, au porojoporojo?
2. Maendeleo pamoja, SADC ni lengo lao,
Biashara ya pamoja, nalo hilo lengo lao,
Mbona mmojammoja, afanya kinyume chao,
Hivi SADC wamoja, au porojoporojo?
3. Ya kwamba bidhaa zao, zile za kilimo chao,
Kwamba zisifike kwao, wabakie wale wao,
Ndio msimamo wao, vikwazo wao kwa wao,
Hivi SADC wamoja, au porojoporojo?
4. Yaloanzishwa Malawi, ule msimamo wao,
Ni mshituko wa kawi, hasa kwa jirani zao,
Shina kuvunjwa matawi, kwa uzalishaji wao,
Hivi SADC wamoja, au porojoporojo?
5. Na Afrika ya Kusini, wakuja na sera zao,
Mazao kwenda bondeni, ni hadi watake wao,
Ya kwao yaje nchini, kama twawagwaya wao,
Hivi SADC wamoja, au porojoporojo?
6. Tanzania ni mwenzao, kwenye jumuiya yao,
Bidhaa kutoka kwao, wanasafirisha wao,
Ila zetu kwenda kwao, waweza vikwazo vyao,
Hivi SADC wamoja, au porojoporojo?
7. Litoa onyo waziri, huo msimamo wao,
Jambo tunalofikiri, ni bora kwetu na kwao,
Wanaonesha kiburi, wamekula ngumu wao,
Hivi SADC wamoja, au porojoporojo?
8. Wiki nzima walipewa, wabadili mwendo wao,
Mazao kuruhusiwa, kuingia nchi zao,
Nchi imepotezewa, huko kunyamaa kwao,
Hivi SADC wamoja, au porojoporojo?
9. Walikwishamwaga mboga, kwamba wafaidi wao,
Sisi tukazugazuga, zirudi akili zao,
Si kwamba wameturoga, yale wafanyayo wao,
Hivi SADC wamoja, au porojoporojo?
10. Huko kula ngumu kwao, na hivyo vikwazo vyao,
Imekuwa zamu yao, kumwaga ugali wao,
Tukosi sisi na wao, vyetuvyetu vyaovyao,
Hivi SADC wamoja, au porojoporojo?
11. Tutabaki hata lini, sisi pamoja na wao,
Kuhusu vya kigeni, kutoka mabara yao,
Badala hapa barani, kuuziana mazao,
Hivi SADC wamoja, au porojoporojo?
12. Afrika yetu ni moja, sisi ni wao kwa wao,
Tushikamane pamoja, kuuziana mazao,
Kama yako ya kupunja, tuketi sisi na wao,
Hivi SADC wamoja, au porojoporojo?
13. Kauzibe kuziweka, kati ya sisi na wao,
Sawa kujipa talaka, kwa vile sisi ni wao,
Vema kuzungumzika, tukumbatiane wao,
Hivi SADC wamoja, au porojoporojo?
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602