ZANZIBAR-Miaka 53 iliyopita Aprili 7, 1972 Rais wa Kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karume aliuwawa kwa kupigwa risasi katika jengo la Makao Makuu ya Chama cha Afro-Shirazi hapo Kisiwandui mjini Zanzibar.
Sheikh Abeid Amani Karume, muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar alizaliwa katika Kitongoji cha Pongwe,Mudiria ya Mwera kisiwani Unguja Agosti 4,1905.
Karume ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia ya watoto watano ya Amani Karume na Amina binti Kadir (Amina Kadudu).
Amani Karume na Amina Binti Kadudu walifunga ndoa huko Mwera. Abeid Amani Karume alizaliwa na ndugu wanne wa baba mmoja na mama mmoja ambao ni wanaume wawili na wanawake wawili.
Lakini wote walifariki kutokana na maradhi mbalimbali na kubaki yeye peke yake.
Baba yake mzazi Abeid Amani Karume alifariki dunia mwaka 1909 wakati Abeid Amani Karume akiwa na umri wa miaka minne.
Abeid Amani Karume alipata elimu ya Kurani na alianza masomo ya msingi katika skuli ya Mwera mwaka aliofariki baba yake wa 1909,ambapo darasa lao lilikuwa la kwanza kuifungua skuli hiyo.
Katika mwaka 1913 wakati akiwa na umri wa miaka 8 mama yake mzazi alimpeleka mjini Unguja kuendelea na masomo.
Huko aliishi na mjomba wake aliyekuwa Sajenti katika jeshi la polisi la King African Rifle (KAR).
Kwa bahati mbaya muda wake wote wa masomo ulikuwa miaka mitatu. Akiwa mjini Zanzibar, Abeid Karume alipata marafiki kadhaa na kuvutiwa mno na harakati za bandari ya Zanzibar.
Kwa wakati huo, bandari ya Zanzibar ndiyo iliyokuwa kubwa Afrika Mashariki. Pia Zanzibar,ilikuwa ndiyo kituo kikuu cha biashara katika eneo zima la Afrika Mashariki na Maziwa Makuu.
Meli za mataifa ya nje hasa Marekani, Uingereza, Ufaransa na Italia zilitia nanga bandarini Zanzibar kupakia na kupakua bidhaa mbalimbali.
Pia meli nyingi zilifika Zanzibar kuchukua maji safi ya kunywa yatokayo katika chemchem ya Mwanyanya.
Meli hizo zilitoa ajira ya muda ya kusafisha mashine na kupangusa moshi. Mara nyingi mabaharia wa meli hizo waliajiri watoto kuwachukulia vikapu vya kununulia vyakula sokoni na kuwalipa ujira mdogo.
Kwa vile alipendelea kazi ya ubaharia, Abeid Amani Karume alifuatana na bwana mmoja aitwae Juma hadi bandarini.
Alijumuika na watoto kadhaa waliofuata ajira ya muda huko bandarini. Ajira ya muda aliyoipata Karume huko bandarini ilimfanya akutane na mabaharia wa nchi mbalimbali na hivyo kuvutiwa na uzuri wa maisha ya ubaharia ya kusafiri na kuona nchi na watu mbalimbali.
Hali hiyo ilimfanya Karume azidi hamu na ari ya kutafuta kazi ya ubaharia na kumuomba mama yake ruhusa ya kufanya kazi melini.
Mwanzoni mama yake mzazi alikataa shauri hilo. Lakini baadaye alikubali ombi hilo baada ya kufahamishwa kuwa meli atakayofanyakazi mwanawe haitosafiri mbali na itatia nanga bandarini Zanzibar mara kwa mara.
Katika mwaka 1919 Abeid Amani Karume alipeleka barua ya kuomba kazi melini, lakini alikataliwa kwa vile alikuwa na umri mdogo wa miaka 14.
Hata hivyo, hakuvunjika moyo na hakurudi Mwera kwa mama yake bali alimtembelea mara kwa mara. Alijiunga na timu za masumbwi na mpira wa miguu na kujuana na watu mbalimbali.
Kwa wakati huo timu za mpira wa miguu zilizojulikana Unguja zilikuwa ni timu ya skuli ya Kiungani iliyoanzishwa na Mwalimu Augostino Ramadhani na John Majaliwa.
Mara nyingi timu hiyo ilishindana na timu ya watumishi serikalini. Baadaye kuliundwa timu nyingine za mpira wa miguu ambazo ni Vuga Boys, New Generation,United Service na New Kings.
Karume alijiungana timu ya New Generation na kucheza nafasi ya mstari wa mbele kushoto Inside left.
Baadhi ya waanzilishi wa timu hiyo ni Bwana Malingumu,Shaaban Feruzi, Saad Shoka, Masoud Thani na Mzee wa Shangani.
Mara tu baada ya kujiunga na timu hiyo,Karume alichaguliwa kuwa msaidizi nahodha.
Katika mwaka 1920 Abeid Amani Karume alikubaliwa kuwa baharia katika meli iliyoitwa Golden Crown (Taji la Dhahabu).
Meli hiyo ilichukua abiria na mizigo kati ya bandari ya Zanzibar, Dar es Salaam, Pemba, Tanga, Mombasa na Mikindani huko Kilwa.
Baadaye alishuka katika meli hiyo na kufanya kazi katika meli nyingine iliyoitwa Cheko.
Kwa bahati mbaya, meli hiyo iligonga mwamba na kuvunjika huko Kimbiji, nje kidogo ya Dar es Salaam lakini watu wote walinusurika.
Kazi ya ubaharia ilimpa tija Abeid Amani Karume kwani alinunua nyumba na viwanja kila alipopata nafasi ya kwenda nyumbani.
Kwa muda wote huo Abeid Amani Karume alifanya kazi katika meli zilizopata leseni ya kufanya kazi katika mwambao wa Afrika Mashariki.
Katika mwaka 1922, akiwa na umri wa miaka kumi na saba, Abeid Amani Karume alipata kazi katika meli ya kampuni ya British Indian Steam Navigation Company ya Uingereza.
Akiwa na kampuni hiyo Karume, alikaa nje miaka mitatu hadi 1925, aliporejea nyumbani kwa mapumziko.
Tayari wakati huo, Karume alikwishatembelea nchi za Japan, Comoro, Madagascar, China, Singapore, NewZealand, Uingereza, Marekani, Canada, Ufaransa, Ubelgiji, India, Ureno, Hispania, Arabuni, Italia na UJgiriki.
Baada ya kupumzika kwa muda, Abeid Amani Karume alijiunga na kampuni ya Eastern Telegraph Company na kufanya kazi katika meli ya kampuni hiyo iitwayo Caranja.
Meli hiyo ilikuwa ikitandika waya za simu
baharini kati ya Zanzibar na Aden. Aliendelea nakazi ya ubaharia hadi mwaka 1938 alipoacha kazi hiyo kutokana na sababu mbalimbali.
Karume alishauriwa na mama yake mzazi kuacha kazi hiyo.Vilevile aliacha kazi hiyo kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama duniani.
Wakati huo,tayari vita vikuu vya pili vya dunia vilikaribia. Baadhi ya kazi alizofanya katika meli hizo ni Greaser, Fireman, Sailor na Headsailor.
Katika kipindi fulani cha kazi yake ya ubaharia, Abeid Amani Karume alifanya kazi chombo kimoja na Khamis Heri Ayemba kutoka Tanga.
Wote wawili walirudi nyumbani wakati vita vya pili vya na baada ya kuacha kazi hiyo,Khamis Heri Ayemba alijihusisha na biashara huko kwao Tanga na kuwa tajiri mkubwa.
Wakati wa kudai uhuru,Ayemba alishirikiana na Peter Muhandona Mwalimu Kihere kuunda tawi la TANU huko Tanga.
Oktoba 23, 1955 wanachama wa mwanzo wa TANU huko Tanga walikutana kuchagua uongozi wa chama hicho.
Katika uchaguzi huo, Khamis Heri Ayemba alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na Peter Muhando alichaguliwa kuwa katibu.
Kutokana na kusafiri sehemu mbalimbali duniani,Abeid Amani Karume alijifunza mengi ya kimaisha na kuona jinsi gani mataifa ya Ulaya na nchi za Afrika.
Katika safari zake za ubaharia alikumbana na matatizo kadhaa.Tatizo kubwa zaidi alilokumbana nalo ni dhoruba kali sana iliyoikumba meli yao wakati wakitokea Australia kwenda Lorencé Marques (Msumbiji).
Katika miaka ya 1930,timu za mpira wa miguu Zanzibar zilikabiliwa na mgawanyiko. Kutoka na na mgawanyiko huo,ndipo hapo mwaka 1931 timu zote za New Kings, Vuga Boys, United Service na New Generation zilipoungana na kuunda umoja wa michezo wa Waafrika uloitwa "African Sports Club".
Timu hiyo ilikuwa na "A" na "B", ambapo Karume alikuwa timu "A" iliyokuwa ya kwanza mwaka huo kwenda Tanganyika kucheza mechi ya kirafiki.
Umoja huo haukwishia hapo kwani katika mwaka 1934 uliundwa umoja wa Waafrika (African Association).
Umoja huo wa Waafrika ndiyo ulogeuka kutoka kwenye michezo na kuwa umoja wa kisiasa.
Katika mwaka 1938 bandarini Zanzibar palikuwa na vijana wa Kiafrika waliounda umoja uliyoitwa "Motorboats Association".
Vijana hao walikuwa wakivusha abiria kutoka bandarini hadi melini kwa kutumia mashua, kazi ambayo iliwasaidia kupata pesa chache za kujiendeshea maisha.
Lakini baadaye walijitokeza wafanyabiashara wajanja wenye asili ya Asia wenye uwezo na kununua boti za mashine na kuvusha abiria.
Wafanyabiashara hao, walitumia mbinu ya kuungana na waafrika katika biashara hiyo.
Baada ya muda mfupi wafanyabiashara hao wenye asili ya Asia waliunda chama chao kilichoitwa Syndicate.
Taratibu wafanyabiashara hao waliwaingiza ndugu zao na wale waafrika waanzilishi waligeuzwa vibarua na kulipwa ujira mdogo sana.
Abeid Karume aliwakusanya kufanya mapatano na waasia hao. Wamiliki wa maboti hao,walikubali kuwalipa waafrika asimilia 40% ya mapato yote na wao walichukua asilimia 60% na kugharamia uendeshaji na matengenezo ya boti hizo.
Baada ya mafanikio hayo Abeid Amani Karume alipata sifa nyingi na mwaka 1939 alianzisha harakati za kuunda chama cha mabaharia Zanzibar ili kupigania haki za wafanyakazi hao.
Kwa wakati huo ilikuwa vigumu sana kuwashawishi watu wasiojua mipango ya vyama vya wafanyakazi.
Hivyo basi mwishoni mwa mwaka huo wa 1939 baadhi ya wafanyakazi walioshauriwa kuanzisha umoja huo walikataa kushiriki katika umoja huo.
Karume hakusita na juhudi zake za kuanzisha umoja huo. Mwaka 1939, alionana na mzungu aitwaye Bwana Douglas Basil Berber aliyekuwa Inspekta wa polisi kuomba kibali cha kuanzisha chama cha mabaharia wa Unguja na Pemba.
Mzungu huyo alimshauri Abeid Karume awakusanye wale wote wanaotaka kuanzisha chama hicho na wajiunge kwa mujibu wa sheria za India.
Zanzibar kwa wakati huo haikuwa na sheria kuhusu vyama vya wafanyakazi Waafrika. Baada ya kuwashauri wenzake,Abeid Karume;