WARSAW-Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameishukuru Serikali ya Poland kupitia Shirika lake la Bima (KUKE), kwa kuonesha nia ya kudhamini upatikanaji wa fedha kwa ajili ya Ujenzi wa kipande cha 3 na cha 4 cha Mradi wa Reli ya Kisasa wa SGR kuanzia Makutupora hadi Tabora na kinachoanzia Tabora hadi Isaka.

Alisema kuwa upatikanaji wa fedha hizo utawezesha ukamilishaji kipande cha 3 (lot 3) cha reli chenye urefu wa km 294, kutoka Makututupora ya mkoani Singida hadi Tabora na kipande kingine cha 4 (lot 4) chenye urefu wa kilometa 130, kutoka Tabora hadi Isaka.


Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali inatafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali ili kuwezesha kukamilisha mradi huo mkubwa wa kimkakati na kuishukuru Poland, Kupitia Shirika lake la Bima (KUKE) kwa kuitafutia Serikali fedha za kukamilisha mradi huo utakaochangia kukuza biashara, ajira na hatimaye uchumi wa wananchi na nchi husika zinazoguswa na miundombinu ya Reli hiyo.
Aidha, katika kikao chao, aliliomba Shirika hilo kuwashawishi wawekezaji kutoka Poland kushirikiana na Serikali pamoja na Sekta Binafsi ya Tanzania kuwekeza katika miradi mingine yenye tija hususan katika sekta za kilimo, nishati, maji, afya, utalii na ujenzi wa miundombinu mingine ya viwanda vya uzalishaji bidhaa kwa faida ya nchi hizo mbili kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Poland (KUKE), Bw. Janusz Wladyczak, alibainisha kuwa Poland iko tayari kushiriki katika Ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR kutokana na umuhimu wake kiuchumi kwa Tanzania na nchi Jirani na kuahidi kuwa Poland iko tayari pia kushirikiana na Tanzania kwenye miradi mingine ya maendeleo kupitia Serikali kwa Serikali na wawekezaji binafsi.
Alisema kuwa nchi yake imebobea katika kilimo, uzalishaji wa bidhaa za mifugo, teknolojia ya nishati, madini na bidhaa nyingine kadha wa kadha zinazozalishwa kwa gharama nafuu na ubora wa hali ya juu na kwamba wawekezaji kutoka nchini humo wako tayari kuwekeza Tanzania.