Rais Dkt.Mwinyi afunga rasmi ziara ya Mabalozi kwenye vivutio vya utalii

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameifunga rasmi ziara ya Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii Tanzania Bara na Zanzibar ijulikanayo kama ‘Diplomatic Safari and Tour’.
Akizungumza katika hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Aldiana, Kizimkazi usiku wa Aprili 14, 2025, ambapo pamoja na masuala mengine Rais Mwinyi amewashukuru Mabalozi kwa kutembelea vivutio hivyo na kuwa mabalozi wazuri wa kuutangaza utalii wa Tanzania.
Aidha, ameeleza mafanikio yaliyofanywa Zanzibar katika kukuza sekta ya utalii ikiwemo upanuzi wa ‘Terminal 3’ katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Abeid Amani Karume uliowezesha kupokea ndege kutoka takribani kampuni za ndege 34 za kimataifa zinazofanya safari za moja kwa moja kuja na kutoka Zanzibar kila mwaka zikiwa na makundi ya watalii wanaokuja kuzuru vivutio vya utalii Tanzania.

Zanzibar ni kivutio cha utalii kinachotambulika kimataifa. Mwaka huu Zanzibar imetunukiwa na ‘World Travels Awards’ kama ‘Africa’s Leading Festival and Event Destination 2024’, ikiwa ni ishara ya kutambulika na kufahamika zaidi kwa Zanzibar ulimwenguni.
“Tunapotazama mbele, dira yetu kwa Zanzibar iko wazi. Tumejidhatiti kujenga sekta ya utalii ambayo sio tu yenye ustawi lakini pia endelevu, jumuishi na yenye kuleta matokeo chanya,” amesema rais Mwinyi.

Aidha, ameeleza kuwa Zanzibar itaendelea kuzitunza malikale zake na kualika wawekezaji kushirikiana katika hili huku akiishukuru Serikali ya Oman ambayo imekuwa ikishirikiana na Zanzibar katika hatua hii.

Ziara hii ilizinduliwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam Aprili 11, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Doto Biteko (Mb.)
Wakati huo huo, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga ameipongeza Wizara ya Mambo ya Nje kwa kuweka mkakati huu wa kutangaza utalii kwa kutumia wanadiplomasia na kuitambua Zanzibar kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya ziara hiyo.

Pia ameeleza katika siku zijazo ni vema ziara hiyo ikaongezwa siku ili Mabalozi waweze kutembelea maeneo mengi pamoja na kupata muda wa kujifunza masuala mbalimbali yanayohusiana na utalii wa Zanzibar.

Naye Mkuu wa Mabalozi nchini na Balozi wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Ahmada El Badaoui Mohammed Fakhi amemshuku Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) kwa maandalizi mazuri ya ziara hiyo iliyomalizika. Vilevile, akasisitiza kuwa hakuna diplomasia bila urithi na kwamba ni vema tukaendelea kuthamini na kutunza utajiri huo kwakuwa Tanzania ina urithi mkubwa wa utalii akitolea mfano wa maeneo waliyotembelea ambayo ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news