Rais Dkt.Samia azidi kuimarisha huduma ya maji kwa wananchi

KIGOMA-Utendaji mzuri wa kazi hupimwa kwa matokeo yanayopatikana, na ili matokeo yaonekane lazima kuwepo na waangalizi, wasimamizi na wafuatiliaji wa utekelezaji kutokana na kile walichokiona kwa macho na sio kusikia na kuangalia katika makaratsi.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira ikikagua mradi wa majitaka Mpanda, Katavi pamoja na tanki la majisafi katika mradi wa maji wa Munanila – Nyakimue wilaya ya Buhingwe, Kigoma.

Moja ya vipimo hivyo vinaweza kuonekana kupitia thamani ya fedha iliyo tumika kwa kulinganisha na uhalisia wa kazi yenyewe

Katika masuala ya ujenzi wa miradi ya maj na kufikisha huduma ya maji kwa wananchi, Rais wa awamu ya sita, Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan akamtwika dhamana Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Pangani, mkoani Tanga kuiongoza wizara hii inayogusa maisha ya wananachi moja kwa moja ili kuhakikisha azma ya serikali ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini na mjini inatimia bila kikwazo.

Katika kufanikisha hilo Wizara ya Maji inatumia taasisi zake ambazo ni Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa maeneo ya mijini, Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA), Mfuko wa Taifa wa Maji, Pamoja na Chuo cha Maji ili kufanikisha huduma ya upatikanaji wa maji kwa maeneo ya vijijini kufika asilimia 85 na mijini asilimia 95 ifikapo mwezi Disemba 2025.

Matokeo mazuri katika Sekta ya Maji kumechagizwa na usimamizi mzuri unaoweza kutofautisha sekta hiyo ilipotoka na inapoelekea kupitia Kamati ya Kudumu ya Maji na Mazingira inayoo ngozwa na nahodha wake Mwenyekiti Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) ambaye ndiye mwakilishi wa wakazi wa Kalenga katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kamati hiyo inaundwa na jumla ya waheshimiwa wajumbe 21 kutoka Bungeni.

Moja ya kazi kubwa ya kamati hii imekuwa ni ukaguzi wa miradi ya maji ili kujionea utekelezaji wake katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikilinganisha na bajeti ya mwaka wafedha husika, kiasi kilichotengwa na kutumika, kushauri na kuweka msukumo katika masuala yanayohusu majisafi na usafi wa mazingira.

Kwa kipindi hiki kamati imetembelea miradi ya maji katika mikoa ya Tabora,Kigoma na Katavi.

Katika mkoa wa Tabora pamoja na sifa ya kuzalishaji asali kwa wingi kwa upande wa suala la maji mkoa upo kamili.

Miradi iliyotekelezwa na kutoa huduma ya maji kwa wananchi na ile inayoendelea na utekelezaji wake ikiwemo Bwawa la Uyui ambapo kamati ilipata fursa ya kufanya ukaguzi.

Bwawa hilo linajengwa kwa fedha za ndani na kiasi cha Shilingi bilioni nne na linauwezo wa kuhifadhi maji kwa mwaka lita za ujazo bilioni 5.1 na likinufaisha zaidi ya wananchi elfu 90 na hivi sasa utekelezaji wa ujenzi wa bwawa umefika asilimia 60.

Kukamilika kwa bwawa hili kutaongeza hali ya upatikani wa maji katika mkoa wa Tabora.

Umbali wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine katika kukagua utekelezaji wa miradi ya maji hilo halikuwa kikwazo kwa wajumbe wa Kamati ya Maji na Mazingira, na safari iliendelea hadi mwisho wa Reli mkoani Kigoma. 
Safari hii ilikuwa mahususi kufika kukagua ujenzi wa mradi wa maji Munanila-Nyakimue wilayani Buhigwe, mradi ambao utanufaisha vijiji nane.

Hadi sasa, katika mradi huu kazi zilizo fanyika ni pamoja na ununuzi na ulazaji wa bomba, ujenzi wa nyumba tatu za mitambo ya kusukuma maji (pumping house) na ujenzi wa vituo vya umma vinne vya kuchotea maji na tanki kubwa la kuhifadhi maji katika mradi ambao umefikia asilimia 67.

Fedha zilizoleta mabadiliko haya ni fedha za ndani kiasi cha Shilingi bilioni 14.9. Jambo la kutia moyo nikuwa hadi kufika Oktoba 2025 mradi huu unatarajiwa kuwa umekamilika.

Aidha, kutokana na Kamati ya Maji na Mazingira kuona jiografia ya mkoa wa Kigoma ilipendekeza umuhimu wa kutumia chanzo cha ziwa Tanganyika kuwa chanzo cha uhakika cha maji kwa mkoa huo na mikoa jirani ikiwamo Katavi.

Hivyo, Wajumbe wa kamati hiyo katika kuhakikisha huduma ya maji inafika kwa wananchi walipita pori la Kigoma kwenda Katavi kwa umbali wa kilomita 249 bila kukata tamaa, kwa mvua au jua.

Wajumbe wa kamati walipata wasaa wa kuona kazi inayofanyika eneo la ujenzi wa mabwawa ya kutibu majitaka katika manispaa ya Mpanda. Maji safi yanapotumika kiasi kikubwa kinachobaki ni majitaka, huo ndio ukweli. Hivyo miundombinu ya majitaka nayo ni muhimu.

Wataalam wamasuala ya huduma ya maji wanasema kuwa asilimia 80 ya majisafi hubadilika na kuwa majitaka hivyo kutokuwepo kwa miundombinu itakayo weza kuchakata majitaka niwazi kuwa hali ya hewa na mazingira kwa viumbe wote wakiwamo binadamu hayatakuwa safi na kuhatarisha afya za wananchi ikiwamo kuwa chanzo cha magonjwa ya mlipuko kama vile Kipindupindu.

Mabwawa yaliyokaguliwa yana uwezo wa kupokea lita za ujazo 600,000 kwa siku na kutokana na mchakato wake, taka hizo zinaweza kuzalisha mbolea itakayoweza kutumika katika shughuli za kilimo. Thamani ya mradi ni kiasi cha Shilingi bilioni 1.197

Mradi wa majitaka katika manispaa ya Mpanda umejikita katika matumizi ya magari na lengo la serikali nikuweka ujenzi wa mitandao ya majitaka moja kwa moja kutoka katika makazi ya wananchi kuelekea kwenye mabwawa hayo.

Kwa utamaduni wa Afrika, zuri hupongezwa., Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeridhishwa na miradi ya maji katika mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora imetoa pongeze kwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (Mb) na wataalam wa Sekta ya Maji nchini kwa kazi ya kuwafikishia wananchi huduma ya majisafi na salama kwa lengo la kufika asilimia 85 vijijini na 95 mjini kama azma ya serikali inavyoelekeza Pamoja na nia thabiti ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan ya “kumtua mama ndoo ya maji kichwani” inatimia.

Msisitizo umetolewa kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji nchini ujengwe utamaduni wa ulindwaji na utunzwaji wa miundombinu na vyanzo vya maji na kila mwananchi anawajibu wakulinda na kutunza miundombinu na vyanzo vya maji kwa kizazi cha sasa na badae ili tuepuka kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi yanayoweza kusababisha ukame na changamoto ya kukosekana kwa maji kutokana na uharibifu wa miundombinu kwani .Ni jambo lililowazi ‘’MAJI NDIO UHAI WETU’’.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news