DODOMA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi Benki ya Ushirika Tanzania (Coop Bank Tanzania).
"Leo ni siku ya kipekee katika sekta ya kilimo na uchumi wa nchi yetu kwa ujumla, ambapo nimezindua Benki ya Ushirika Tanzania.
"Benki hii ni sehemu ya kazi kubwa tunayoendelea kuifanya ya kuongeza tija katika sekta ya kilimo. Uanzishaji wa benki hii unalenga kutimiza hitaji la wananchi la upatikanaji wa mitaji kwa wakulima, hasa wakulima wadogo walioko vijijini.
"Hatua hii ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (2020-2025) ambapo itachochea zaidi maendeleo nchini ikiwemo ajira kwenye kilimo, ukuaji wa Pato la Taifa, upatikanaji wa malighafi za viwandani na kuhakikisha usalama wa chakula.
"Nimeielekeza benki hii kuwa bunifu katika kutanua wigo wa huduma zake pamoja na kusimamia kikamilifu fedha zinazotolewa, ili kujihakikishia uimara, uwezo wa kujiendesha kibiashara na uendelevu wa benki yenyewe."
Vilevile,Rais Dkt.Samia amesema, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha, itatekeleza mpango muhimu wa maendeleo ya sekta ya fedha, kuboresha mifumo, na kubuni mifumo mpya ya huduma za kifedha.Akizungumza katika Ukumbi wa Mikutano Jakaya Kikwete mara baada ya uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu ya Benki ya Ushirika Tanzania jijini Dodoma, Rais Dkt.Samia amesisitiza kuwa, serikali imechukua hatua madhubuti kuimarisha sekta ya ushirika ili kuongeza uzalishaji, kuhakikisha usalama wa chakula, na kukuza kilimo biashara.
Pia,amesema serikali inajitahidi kutafuta masoko bora kwa mazao ya wakulima na imeanzisha mifumo ya stakabadhi ghalani na minada ili kuhakikisha mkulima anapata haki yake.
Rais Dkt.Samia amesema kwamba,vyama vya ushirika vitakuwa na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yao na kwamba serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Benki ya Ushirika Tanzania.Hivi karibuni, Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe alisema,Benki ya Ushirika Tanzania itaanza na mtaji wa shilingi Billioni 55 ikiwa ni benki ya kwanza nchini inayomilikiwa kwa asilimia 51 na vyama vya ushirika pamoja na wanachama wake na asilimia 49 zinamilikiwa na wadau wengine.
Alisema kuwa, Benki ya Ushirika Tanzania itaanza na Matawi manne ambapo ni katika mikoa ya Dodoma, Mtwara, Kilimanjaro na Tabora na awamu ya pili itakuwa katika mikoa ya Kagera, Mbeya, Mwanza, Dar es Salaam na Katavi.Kupitia Benki ya Ushirika Tanzania (COOP Bank) wanachama wa ushirika wataweza kupata mikopo nafuu, kuhifadhi fedha salama, na kupata elimu ya kifedha kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na ya kitaasisi.
