NA LWAGA MWAMBANDE
REJEA katika neno la Mungu kupitia Biblia Takatifu kitabu cha Yeremia 29:13-14, neno linasema, "Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.
"Nami nitaonekana kwenu, asema BWANA, nami nitawarudisha watu wenu waliofungwa, nami nitawakusanya ninyi, nikiwatoa katika mataifa yote, na katika mahali pote, nilikowafukuza, asema BWANA; nami nitawaleta tena, hata mahali ambapo kutoka hapo naliwafanya mchukuliwe mateka."
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anaweka mkazo kuwa, Ruthu alivyojitoa kwa Naomi ni fundisho kwa ajili yetu kujitoa kwa ajili ya Mungu. Endelea;
¹ Kwa Mungu ni kujitoa, upate mtumikia,
Kwake zaidi ya ndoa, hilo ninakuambia,
Usichukulie poa, kwa kusinziasinzia,
Ruthu alivyojitoa, kwa Naomi ni fundisho.
² Kwenda naye mama mkwe, bila nyuma angalia,
Kwamba mabaya wafikwe, kwake aweze tulia,
Huko na huko atakwe, abaki amwangalia,
Ruthu alivyojitoa, kwa Naomi ni fundisho.
³ Huyu ni mmataifa, kwao ngeweza bakia,
Hapa anapata sifa, alivyojiamulia,
Kwamba kupona na kufa, kwa Naomi liingia,
Ruthu alivyojitoa, kwa Naomi ni fundisho.
⁴ Ndugu hakufikiria, mume hakutarajia,
Yeye alishika njia, bila nyuma angalia,
Naomi likofikia, naye ndiko litulia,
Ruthu alivyojitoa, kwa Naomi ni fundisho.
⁵ Ni Ruthu siyo mwenzake, mkataba lo ingia,
Kubaki na mkwe wake, pasi hata kumwachia,
Alichomoa mwenzake, na kwao akabakia,
Ruthu alivyojitoa, kwa Naomi ni fundisho.
⁶ Ndiyo hivyo hata sasa, katika yetu dunia,
Hata kuwe na hamasa, imani kushikilia,
Watu wanagusagusa, wala si kushikilia,
Ruthu alivyojitoa, kwa Naomi ni fundisho.
⁷ Badala ya kujitoa, Mungu kumtumikia,
Watu wanajiondoa, na yao kukimbilia,
Wadhani wajiokoa, kumbe wanadidimia,
Ruthu alivyojitoa, kwa Naomi ni fundisho.
⁸ Kazi inajitokeza, kazi yake kuingia,
Watu wajibaraguza, wakute ishaishia,
Ndipo wanajitokeza, tuone livyovalia,
Ruthu alivyojitoa, kwa Naomi ni fundisho.
⁹ Ruthu alivyojitoa, mkwewe kumwandamia,
Funzo nasi kujitoa, Mungu kumtumikia,
Hapo tunajiokoa, na kukaa kwake njia,
Ruthu alivyojitoa, kwa Naomi ni fundisho.
¹⁰ Kwa moyo wao jitoe, Mungu kumtumikia,
Kwa roho yako jitoe, Mungu kumtumikia,
Kwa nguvu zako jitoe, kazi ukimfanyia,
Ruthu alivyojitoa, kwa Naomi ni fundisho.
¹¹Akili alizokupa, si kutanga na dunia,
Vema Mungu kumlipa, jinsi unazitumia,
Jua hiyo inalipa, chini huwezi bakia,
Ruthu alivyojitoa, kwa Naomi ni fundisho.
¹² Jinsi unavyojitoa, Mungu kumtumikia,
Na Yeye atajitoa, wewe kukusaidia,
Yako yatakuwa poa, ya mbinguni na dunia,
Ruthu alivyojitoa, kwa Naomi ni fundisho.
(Ruthu 1:8-18)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
@Moto Ulao Online Church