Simba SC yaingia mkataba wa shilingi bilioni 38.12 na Jayrutty utengenezaji na usambazaji wa jezi na vifaa

DAR-Kampuni ya Jayrutty Investment Company Limited ambayo imeshinda tenda ya utengenezaji na usambazaji wa jezi na vifaa vyenye nembo ya Simba Sports Club imesema jambo la kwanza inakwenda kutekeleza ni kujenga uwanja wa mpira ambao utachukua mashabiki 10,000 hadi 12,000.
Uwanja huo unatarajiwa kujengwa Bunju jijini Dar es Salaam kama Simba Sc watapendekeza hivyo.

Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Jayrutty Investment Company Limited, CPA Joseph Rwegasira ameyasena hayo Aprili 16,2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya kusaini kandarasi ya miaka mitano na klabu hiyo.

"Simba ni timu kubwa Afrika na sisi tumesema kwamba tutanunua basi jipya la Irizar, kila kitu kipo sawa. Muda si mrefu mtaliona hapa. Tutaangalia pia upande wa media, tunakwenda kujenga media kubwa kama klabu zingine kubwa na tumeshaanza utaratibu.
"Tunajua kwamba Simba makao makuu yapo Msimbazi,lakini tunakwenda kujenga ofisi za kisasa.

"Lakini pia kila mwaka tutatoa Tsh. 100 milioni ya kusaidia kukuza soka la vijana. Kila mwaka pia tutachangia Tsh. 100 milioni kuchangilia pre-season.

"Pia tumeahidi kujenga kituo maalumu cha matibabu ya wachezaji. Kila mwaka pia tutashiriki bega bega katika Simba Day, tutachangia Tsh. 100 milioni kila mwaka,"amesema CPA Rwegasira.

Pia CPA Rwegasira amesema kuwa,"Hizi ni baadhi ya faida za ziada ambazo sisi tutatoa kwa Simba Sports Club.

"Kila mwaka tumekubali kutoa Tsh. 470 milioni kwa wachezaji, uongozi utagawa kwa namna ambayo wataona inafaa na hii fedha itakuwa inaongezeka kila mwaka.

Hatua hiyo inakuja wakati mkataba wa miaka miwili wa Kampuni ya Sandaland kuhusu uzalishaji wa vifaa vya michezo kwa Club ya Simba SC ukiwa unaelekea ukingoni.

Kampuni ya Jayrutty itakuwa ndio mzalishaji na muuzaji mpya wa jezi zao kwa kipindi cha miaka mitano katika mkataba huo wenye thamani ya shilingi Bilioni 38.12.

Pengine,mkataba huu mpya unakuwa mkataba ulioweka rekodi ya kipekee kwa Tanzania na Afrika Mashariki,kwani imeelezwa kuwa hakuna klabu yoyote ya soka yenye mkataba wa thamani hiyo.

Mwaka 2019 Simba iliingia mkataba wa miaka miwili na UhlSport wenye thamani ya shilingi milioni 600.

Aidha,mwaka 2021 wakasaini mkataba wa miaka miwili na Vunjabei wenye thamani ya shilingi Bilioni 2 na mwaka 2023 waliingia mkataba wa miaka miwili na Sandaland wenye thamani ya shilingi bilioni 4.

"Tumeingia mkataba wa kimataifa na brand mojawapo kubwa duniani ambayo inazivisha klabu nyingi kubwa.
“Mwaka huu na miaka inayofata mambo yatakuwa mazuri sana, tunakuja kuonyesha tofauti.

"Tutahakikisha Simba inapata thamani kubwa kulingana na ukubwa wake ndio maana tumewekeza fedha nyingi sana kwenye hili.

"Kwa mara ya kwanza Simba Sports Club itakuwa klabu ya kwanza Tanzania kuvaa jezi ambayo ni internationa brand.

"Naomba kuwaambia kuanzia sasa mtakuwa na furaha isiyo na kifani. Kwa ushirikiano tulionao na uongozi tutahakikisha Simba inarudisha heshima yake sio tu nchini, Afrika na duniani. Nawashukuru sana Simba kwa kutuamini.

“Hivi karibuni tutaitangaza brand ambayo itavalisha jezi. Tutapata ubora wa hali ya juu katika bei rafiki kabisa, kama Mwanasimba jivunie, kama uliweza kununua jezi zilizopita basi hata hivi utaweza.
"Nitoe pongezi kwa wazabuni waliopita, nitoe pongezi kwa VunjaBei, nitoe shukrani kwa Sandaland na kubwa tuendelee kushirikiana,"alifafanua Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Jayrutty Investment Company Limited, CPA Joseph Rwegasira.

Ameendelea kufafanua kuwa, “Kiasi ambacho kimetajwa ni kiasi ambacho tumezingatia mambo mengi kama klabu.

"Nipende kuwahakikishia kabla hata hatujafanya kitu chochote tumeshaweka asilimia 30 ya hiki kiasi cha mwaka wa kwanza.

“Jambo la kwanza ambalo tunakwenda kutekeleza ni kujenga uwanja wa mpira, uwanja ambao utachukua mashabiki 10,000 hadi 12,000.

Serikali

Kwa upande wake mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.Hamis Mwinjuma amesema,“Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu imewekeza sana kwenye michezo na hasa mchezo huu pendwa wa mpira wa miguu.
"Kitakwimu hakuna kipindi tumefanya vizuri kama kipindi hiki. Mchezo huu unaendelea kutupa raha mioyoni na kututangaza nje ya mipaka ya nchi.

“Hili nililosikia leo la ujenzi wa uwanja limenivutia sana. Mkiwa na kiwanja cha watu 10,000 au 12,000 kinaweza kutumika kwa michezo ya ndani, michezo ya nje ndio mkawa mnatumia Uwanja wa Mkapa, mtaupunguzia hata majukumu.

“Itoshe kusema ni uwekezaji wa mkakati ambao umekuja wakati sahihi. Serikali kama mlezi wetu tunawapongeza sana.
“Naamini mna maarifa ya kucheza mchezo wa nusu fainali utakaochezwa Zanzibar na kule Afrika Kusini na kuhakikisha mnavuka na kuingia fainali hadi kushinda ubingwa wa Afrika.

"Na sisi kama serikali kama mara zote ambavyo tunawaunga mkono hatutawaacha hata wakati huu. Tupo nyuma yenu kuhakikisha mnashinda ubingwa wa Afrika. Hatuishii hapa.”

Uongozi Simba SC

Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu amesema,“Kamati ya Tenda iliundwa na wenyeviti wa kamati ndogo za bodi.

"Mimi nawapongeza sana wajumbe hawa kwa kazi kubwa waliyofanya kwa niaba ya bodi. Bodi nzima iliridhia kwamba hakuna sababu aliyeshinda kutokupewa hii tenda.
“Mapinduzi makubwa ya jezi yalifanywa na Kassim Dewji kwa zaidi ya miaka 10. Miaka hiyo tulikuwa tunaletewa tu jezi nyeupe na nyekundu, lakini yeye akaleta jambo la tofauti lakini game changer ni VunjaBei yeye ndio alikuja kuonyesha njia, Sandaland alifanya kazi yake, lakini sasa amekuja Jayrutty.

“Umeahidi mambo mengi uyafanyie kazi usijesema kwamba ulitamani brand kubwa, lakini imeshindakana. Nawahakikishia Wanasimba wote tutashirikiana kufanikisha hilo.

"Tutashirikiana na mpango wa mwekezaji Mohammed Dewji, hivyo hakutakuwa na kuingiliana katika utekelezaji wake,"amesema Mwenyekiti wa Klabu, Murtaza Mangungu.

Kamati ya Tenda

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Kamati ya Tenda wa Simba SC, Dkt.Seif Muba alisema, “Tulipokea barua nyingi za maombi,lakini bodi iliamua makampuni yashindane kwa tenda. "Kampuni nane zilichukua tender document lakini kampuni sita zilirudisha document. Maombi ya wazabuni yalifunguliwa kwa uwazi na baada ya mchakato wazabuni wote walijulishwa mzabuni ambaye ameibuka mshindi kwa kuweka fedha na vitu vingi ambavyo tulihitaji. Tuliingia mkataba wa miaka mitano na kampuni hiyo.

“Mshindi aliyeshinda tenda hiyo ameshinda kwa kuweka kiasi cha fedha cha shilingi 38 Bilioni. Napenda kuitangaza kampuni ya Jayrutty Investment Company Limited kama mshindi. Klabu ya Simba inakwenda kupata shilingi 5.6 Bilioni kwa mwaka.”

Msemaji wa Simba

Naye Msemaji Mkuu wa Simba SC,Ahmed Ally amesema,“Jambo ambalo linanyika hii leo ni jambo ambalo tumelitamani kwa muda mrefu lakini leo limekamilika.
“Timu ya vijana inafanya mazoezi kwenye uwanja wa kukodi, timu ya wanawake inafanya mazoezi kwenye uwanja wa kukodi ni senior team peke yake ndio inafanya mazoezi Mo Simba Arena, Bunju.

"Wanaokodisha waanze kutafuta wateja wengine. Inakuja ndinga mpya, ipo timu wanayo, lakini yao itakuwa ya zamani, yetu itakuwa mpya zaidi.

“Wakati tunaipongeza kampuni ya Jayrutty, tuipongeze pia kamati ya tenda na Bodi ya Wakurugenzi kwa kuwa na mawazo ya kuichagua Jayrutty.

"Wangekuwa ni viongozi wanaojali maslahi yao wangechangua yeyote, lakini sababu wameweka maslahi ya Simba mbele wamemchagua Jayrutty na kumpa mkataba wa miaka mitano ili afanye kile alichokusudia ili Simba izidi kwenda kimataifa.
“Moja ya ahadi ni kujenga ofisi mpya, watu wa menejimenti ya Simba muanze kushangilia. Mimi mkijenga ofisi mpya naomba unijengee ofisi ya peke yangu.

"Lakini pia tunajengewa ofisi ya media ni jambo la kupongeza. Kwa sasa tunaongoza mitandao yote ya kijamii na hapo bado hatujajengewa studio. Kwa sasa mpinzani wetu ni Al Ahly na Zamalek, lakini kwa studio hii tunakwenda kuwapita.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news