Simba SC yatinga fainali CAF Confederation Cup

DURBAN-Matokeo ya bila kufungana katika dimba la Moses Mabhida Stadium lililopo mjini Durban nchini Afrika Kusini kati ya Simba Sports Club ya Tanzania na Stellenbosch FC ya Afrika Kusini yamewashangaza wengi.
Mshangao huo wa leo Aprili 27,2025 umekuja baada ya Simba SC kuandika historia kubwa barani Afrika.

Ni kwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF Confederation Cup) ambapo wameiondoa Stellenbosch FC kwa jumla ya mabao 1-0.

Aidha,hii ni mara ya pili Simba SC kufika hatua ya fainali ya michuano ya CAF, baada ya mara ya kwanza kufanya hivyo mwaka 1993.

Katika mtanange huo, Simba SC wameingia wakiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa bao moja walilopata kwenye mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa katika Uwanja wa Amaan Zanzibar, Aprili 20,2025.
Awali Kocha Mkuu, Fadlu Davids aliwasisitiza wachezaji kuwa makini muda wote kuhakikisha hawafanyi makosa ambayo yatapelekea kuruhusu bao.

“Tuna kibarua kigumu lakini malengo yetu ni kuhakikisha tunavuka na kutinga fainali. Tunahitaji sare ya aina yoyote kama ikishindikana kabisa hata bila kufungana, lakini tumejipanga kutafuta bao la ugenini ili kuwapa wakati mgumu wapinzani,” amesema Fadlu.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji kabla ya mchezo huo mshambuliaji Steven Mukwala alisema katika mchezo wa mkondo wa kwanza waliibuka na ushindi wa bao moja kule Zanzibar na wanahitaji kuulinda ili kupata nafasi ya kutinga fainali.
“Bado kuna dakika 90 za kupambana ili kufikia malengo yetu tuliyojiwekea. Bao moja tuliloshinda nyumbani hatuwezi kusema limetuvusha moja kwa moja tupo tayari kupambana hadi mwisho kuona tunaweza kufika fainali,” alisema Mukwala.

Kwa sasa Simba SC wanasubiri kumenyana na mshindi kati ya CS Constantine ya Algeria na RS Berkane ya Morocco katika fainali ya kwanza ambayo itapigwa Mei 17, 2025 huku mchezo wa marudiano ukipangwa kuchezwa Mei 25, 2025.

CAF Confederation Cup lilianzishwa mwaka 2004 baada ya kuunganishwa kwa michuano ya African Cup Winners' Cup iliyodumu kuanzia mwaka 1975 na CAF Cup iliyoanzishwa mwaka 1992.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news