DURBAN-Kocha Mkuu wa Simba Sports Club, Fadlu Davids amesema,hawatakiwi kushangilia sana kwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika na badala yake wanahitaji kutunza nguvu kwa ajili ya fainali.

Fadlu amesema alitegemea mechi ngumu kutoka kwa Stellenbosch, lakini waliweza kudhibiti presha waliyotupa na kufanikiwa kutinga fainali.
Aprili 27,2025 kikosi cha Simba SC imefanikiwa kutinga fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Stellenbosch.
Ni katika mchezo wa nusu fainali ya pili uliopigwa Uwanja wa Moses Mabhida jijini Durban.
Simba SC imefanikiwa kutinga fainali kwa jumla ya bao moja kufuatia ushindi wa bao moja walilopata kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Amaan Zanzibar,Aprili 20,2025.
Mchezo ulianza kwa kasi ya kawaida huku wenyeji Stellenbosch wakifika langoni kwa Simba SC mara kadhaa, lakini walikuwa imara kuhakikisha wanaendelea kuwa salama.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku timu zikishambuliana kwa zamu ambapo dakika ya 55 kupitia usaidizi wa VAR mwamuzi alikataa mkwaju wa penalti ambapo alidhani Karabou Chamou ameshika ndani ya 18.
Aidha,Kocha Mkuu, Fadlu Davids alipanga kikosi kile kile kilichocheza mechi ya mkondo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Amaan Zanzibar, Aprili 20 walioibuka na ushindi wa bao moja.
Hiki hapa kikosi kamili kilichopangwa:
Moussa Camara (40), Shomari Kapombe (12), Mohamed Hussein (15), Karaboue Chamou (2), Abdurazak Hamza (14), Yusuph Kagoma (21), Kibu Denis (38), Fabrice Ngoma (6), Steve Mukwala (11), Jean Charles Ahoua (10), Elie Mpanzu (34).
Wachezaji wa Akiba:
Ally Salim (1), David Kameta (3), Valentine Nouma (29), Edwin Balua (37), Debora Fernandes (17), Awesu Awesu (23), Leonel Ateba (13), Che Fondoh Malone (20).