NA DR MOHAMED MAGUO
LEO Aprili 27,2025 timu ya Simba ya Tanzania imefuzu kuingia fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF Confederation Cup) kwa kuiondosha timu ya Stellenbosch FC ya Afrika ya Kusini.

Hakika Simba ni timu Bora fahari ya Tanzania. Mchezo wa marudiano umechezwa leo Moses Mabhida Stadium mjini Durban nchini Afrika Kusini na kutoka sare ya kutofungana. Endelea na utenzi huu hapa chini ujifunze jambo;
¹Kwa ukanda wa Afrika
Ya kati na masharika
Ni simba inayoshika
Namba moja kwa ubora
²Simba hii kwa hakika
Ni ngumu kukamatika
Kila siku yasifika
Magoli kutumbukiza
³Mashabiki wanacheka
Furaha isosemeka
Kwamba Simba imefika
Fainali kwa kishindo
⁴Simba i pamechimbika
Hata Sauzifrika
Steleboshi ametoka
Ubaya jama ubwela
⁵Steleboshi nyakanyaka
Kwa mnyama 'meshikika
Masare yamesambuka
Mnyama ametoboa
⁶Taifa kuheshimika
Ni Stele kuanguka
Na Simbaye' kusomeka
Fainali 'meingia
⁷Kongole nazipeleka
Msimbazi wakawaka
Heshima mmeiweka
Heko kwenu wana Simba
⁸Simba i twajivunia
Timu yetu Tanzania
Vijana wametimia
Soka la kimataifa
⁹Nguvu moja nakwambia
Ndugu yangu we sikia
Simbaye' tumainia
Kombe italifumbata
¹⁰Watu wote wafurahia
Kwa sana washabikia
Shwangwe wanashangilia
Simba ni mkali sana
MTUNZI
Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mshairi wa Kisasa
Mhadhiri Mwandamizi
Mkuu wa Itifaki
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
27/04/2025