NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Crispin Chalamila amesema,vitendo vya rushwa katika uchaguzi ni kati ya vikwazo vinavyoathiri haki na fursa za wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.
Chalamila ameyasema hayo leo Aprili 29,2025 katika semina maalum iliyoandaliwa na TAKUKURU kwa wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam namna ya kutoa elimu kwa wananchi ili kuepuka vitendo vya rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Aidha,amesema kuwa vyombo vya habari ni wadau muhimu katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa haki na usiohusisha vitendo vya rushwa.
Katika hatua nyingine amesema, katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Kifungu cha 7(b) kimeitaka TAKUKURU kuwashirikisha na kushirikiana na wadau katika kuzuia na kupambana na rushwa.
"Matakwa haya yanazingatia ukweli kuwa, hakuna chombo kimoja kinachoweza kuzuia na kupambana na tatizo la rushwa peke yake."
Kwa muktadha huo, Chalamila amesema TAKUKURU imeona ni busara kwa wadau nchini ikiwemo wahariri wa vyombo vya habari kukutana na kujadili namna ya kuzuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi mkuu.
Amesema,Serikali na taasisi hiyo inatambua kuwa, vyombo vya habari ni wadau muhimu katika kuwezesha kufanikisha uchaguzi wa haki na huru usiokuwa na vitendo vya rushwa.
"Uwepo wenu hapa unadhirisha dhamira yenu ya kupambana na kuzuia rushwa hususani katika kipindi hiki cha mchakato wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu nchini."
Amesema,mamlaka hiyo inatambua umuhimu mkubwa wa tasnia ya habari katika kutoa elimu kwa umma ili waweze kuelewa masuala mbalimbali ikiwemo siasa,sera na demokrasia ya nchi.
Amesema, kukosekana kwa taarifa sahihi kunaweza kusababisha hali ya sintofahamu miongoni mwa jamii, hivyo vyombo vya habari vinajukumu kubwa la kuhakikisha vinatoa taarifa sahihi.
"Uchaguzi ni mchakato ambao unawapa wananchi fursa na haki ya kuchagua viongozi wanaowataka.
"Ni msingi wa demokrasia na ndiyo ambao huwa unatoa taswira namna ambavyo taasisi za Serikali zinatakavyowajibika kwa umma.
"Mwaka huu wa 2025 tutakuwa na Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani na ndiyo maana tukaona tuitane tena ili kwa pamoja tuelimishane na pia tujadili namna ya kuzuia na kupambana na rushwa tubapoelekea kwenye uchaguzi mkuu.
"Kwanza,vyombo vya habari vina jukumu la msingi katika kutoa elimu kwa wananchi."
Amesema, wananchi wengi huwa wanapata taarifa zao kupitia redio,runinga, magazeti na mitandao ya kijamii.
"Hivyo, vyombo vya habari vinaweza kuelimisha kuhusu athari za kupokea rushwa wakati wa uchaguzi na umuhimu wa kuchagua viongozi bora kwa misingi ya sera zao na si kwa misingi ya zawadi au hongo."
Amesema, elimu hiyo ni muhimu imfikie kila mpiga kura.
Pia, ameeleza kuwa, vyombo vya habari vina uwezo mkubwa wa kufikisha taarifa sahihi na kwa haraka kwa wananchi."Ni matarajio yetu kuwa, kupitia warsha hii na kwa makubaliano tutakayoyafikia tutaweza kuwafikia Watanzania wengi zaidi kwa kuwaelimisha kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi."
Vilevile amesema, kupitia uandishi wa habari za kichunguzi waandishi wa habari wanauwezo wa kuchunguza na kubaini viashiria vya rushwa katika mchakato wa uchaguzi.
"Kwa kufanya hivyo, itasaidia kuhimiza uwajibikaji ili kuwafanya viongozi wa taasisi na wagombea kutekeleza majukumu yao kwa uwazi."
Tags
Habari
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
TAKUKURU Tanzania
Uchaguzi Mkuu 2025

