Tuendelee kudumisha amani na utulivu kwa ustawi bora wa jamii na maendeleo nchini-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa, Uchaguzi Mkuu ujao utafanyika kwa amani na utulivu.
Alhaj Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo alipotoa salamu baada ya kujumuika kwa Sala ya Ijumaa katika Masjid Raudha iliyopo Darajabovu Wilaya ya Mjini.

Amesema kuwa,dhamira ya Serikali anayoiongoza ni kuona uchaguzi huo kuwa ni kielelezo cha kuwepo kwa amani ya kudumu hapa nchini na kila mwananchi anapata fursa ya kutekeleza haki ya msingi ya Kikatiba ya kupiga kura.
Rais Alhaj Dkt.Mwinyi amesema,ni wajibu wa msingi wa kila mwananchi kuhakikisha amani iliyopo inadumishwa wakati huu na baada ya uchaguzi ili nchi ipige hatua zaidi za maendeleo katika nyanja tofauti.

Aidha,amewasihi waumini wa Dini ya Kiislamu kuendeleza utaratibu wa kuwasaidia watu wanaohitaji misaada kama ilivyofanyika vema wakati wa Mwezi wa Ramadhani.

Dkt.Mwinyi ameeeleza kuwa,mwenendo mzuri uliotekelezwa wakati wa Ramadhani unapaswa kuendelezwa kwa kiwango kile kile, kwani bado makundi ya wanaohitaji kusaidiwa yapo ndani ya jamii.
Naye Katibu Mtendaji wa Afisi ya Mufti,Sheikh Khalid Ali Mfaume amewahimiza waumini hao umuhimu wa kumuombea dua Kiongozi wa Nchi kwani ni wajibu wa kila Muumini wa Kiislamu.

Amesema kuwa, kutengemaa kwa Kiongozi ndio nyenzo muhimu na dira ya mafanikio ya Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news