NA GODFREY NNKO
TUME ya TEHAMA nchini imesema, inaratibu programu mbalimbali ambazo ni mahususi kwa ajili ya kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania ambao ni wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
“Wataalamu wa TEHAMA ambao wanatoka vyuoni wanaingia kwenye uzalishaji, kwenye taasisi au kwenye makampuni, kwa hiyo tunazo programu maalumu ambazo ni mahususi kwa ajili ya kukuza uwezo wao;
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Wataalamu wa TEHAMA kutoka Tume ya TEHAMA nchini, Sadath Kalolo ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa mahojiano maalum katika kipindi cha Baragumu cha runinga ya Chanel Ten.
Pia, amesema wana programu ambazo zina uwezo wa kukuza uelewa wa TEHAMA hasa kwa watumiaji kwa sababu ili teknolojia iweze kuyanufaisha makundi yote ya jamii lazima yawe na uwezo wa kuitumia.
“Hata wale watoto ambao wapo kwenye shule za awali na wao wana programu ambazo zinawafaa wao ili waweze kuanza kuipokea TEHAMA katika maisha yao.”
Bidhaa
Katika hatua nyingine, Kalolo amesema ili tuweze kunufaika na matumizi ya TEHAMA, lazima tuwe na bidhaa za TEHAMA ambazo zimetengenezwa mahususi kwa matatizo yanayozizunguka jamii zetu.
“Sote tunatumia mifumo ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram na mingineyo ambayo ilitengenezwa na wenzetu huko kwao.
“Sasa, wale wenzetu wakati wanatengeneza walitakiwa wawe wanatatua matatizo ambayo yanazizunguka jamii zao, sasa matatizo ya kwetu sisi, mathalani yaliyopo hapa Kariakoo, wanaoweza kutatua vizuri kabisa ni vijana wetu wa TEHAMA.”
Kalolo amesema, kutokana na hayo, jukumu kubwa ambalo wanalifanya ni kuhakikisha kwamba wanawawekea vijana hao mazingira mazuri ili waweze kjuja na mawazo yatakayoleta bidhaa mpya za TEHAMA.
Amesema, bidhaa hizo ni zile ambazo zitatatua matatizo ambayo jamii ya Watanzania inakutana nayo kila siku iwe ni usafiri, kulipia huduma za kifedha au hududuma nyinginezo.
“Tunataka, suluhisho hizo au bidhaa hizo zitengenezwe na vijana wetu, wakati wakifanya hivyo vijana wenyewe wanajiajiri na wanaajiri wenzao, sasa wakati tunatekeleza hilo, tunafanya mambo mawili.”
Kalolo ameyataja mambo hayo kuwa ni kuwatambua hao wabunifu wa TEHAMA kwa kuwasajili. “Kwa hiyo, mpaka sasa tumesajili kampuni changa zaidi ya 200 ambazo zipo kwenye kanzidata yetu.”
Jambo la pili, Kalolo amesema, Serikali kupitia Tume ya TEHAMA inaanzisha vituo maalumu ambavyo vitasaidia kuwakuza vijana wabunifu wa TEHAMA nchini.
“Hivi vituo,tuna vituo nane ambavyo vinaanzishwa vya kikanda kupitia Mradi wa Benki ya Dunia ambao tunausimamia sisi Tume ya TEHAMA kwa kushirikiana na wizara yetu.”
Amesema, vituo hivyo vinaanzisha Dar es Salaam, Zanzibar, Lindi, Dodoma, Tanga, Arusha, Mbeya na Mwanza. “Vitu hivi vitakuwa ni mahususi kwa ajili ya kuwalea hawa vijana, kuwapa mafunzo maalumu na kuhakikisha kwamba, wanaingia sokoni wakiwa na bidhaa zao ambazo zinakubalika na zinaweza kutumika.”
Pia, amesema wao kama tume hawaishii kwenye vituo vya kikanda kama hivyo, kwani wataanzisha vituo maalum kwa ajili ya kukuza bunifu za TEHAMA kwenye ngazi ya wilaya.
“Tunajua kwamba, vijana wetu wako huko, tuliko toka wilayani humo, sasa lazima tuwe na vituo vidogovidogo ambavyo vitawapokea wakiwa na mawazo tu ya kiubunifu.
“Kijana akiamka leo akasema nina wazo tu la kiubunifu ambalo litatusaidia kuboresha huduma zetu tunazozitumia kama jamii,basi tunampokea kwenye vituo vile, tunampokea tunampa mafunzo maalumu na tutahakikisha anawezeshwa kimtaji ili aweze kuboresha wazo lake na kulipeleka sokoni.”
Akili Unde (AI)
Kuhusu nafasi ya Akili Unde amesema,Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inajumuisha teknolojia nyingi ikiwemo teknolojia zinazoibukia.
“Sasa, Akili Unde ni moja wapo ya teknolojia mpya kabisa ambazo zimeibuka siku za hivi karibuni na zina zina nafasi kubwa ya kuleta mageuzi makubwa kwenye namna tunavyotoa huduma na namna tunavyoendesha uchumi wetu."
Amesema, kutokana na hatua hiyo, Akili Unde ina nafasi kubwa katika jamii, hivyo ni namna ambavyo vijana wataipokea na kuhakikisha inajumuishwa kwenye shughuli za kiuchumi ndivyo tutakavyonufaika nayo.
"Kumekuwa kuna maneno tofauti, wengine wanahofia kwamba labda AI inakuja kuondoa ajira zetu, lakini sisi tunavyojua na kulingana na tafiti tunazozifanya, tunaona kwamba AI ina fursa nyingi ambazo inatuletea kuliko zile chnagamoto ambazo wengine wanahofia kwamba zinaweza kuja."
Wizara
Mkurugenzi Msaidizi,Tafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Wataalamu wa TEHAMA kutoka Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Mhandisi Bahati Zuberi amesema, Sera ya mwaka 2016 inazungumzia umuhimu wa jamii Habari (digital societies).
“Na mabadiliko ya kiteknolojia yanatulazimisha kwenda kwenye uchumi wa kidigitali. Kwa hiyo, kama sera ambayo ndiyo msimamizi mkuu wa Sekta ya Mawasiliano kwa kushirikiana na taasisi zake zilizopo chini ikiwemo TCRA,Tume ya TEHAMA na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi).”
Amesema, wanachokifanya kikubwa ni kuanzisha programu za Kitaifa ili kuhakikisha wanajenga weledi kwa watumiaji wa TEHAMA iweze kuleta mchango na mapinduzi kusudiwa kwenye shughuli za kiuchumi na kijamii.
“Kwa hiyo, ndiyo jukumu kubwa la wizara, lakini wizara haiwezi ikafanya peke yake kwa sababu kama mada inavyozungumzia mazingira wezeshi ya bunifu, tuna wadau wetu wakubwa kwa mfano Wizara ya Elimu, kuna makampuni ya simu, taasisi binafsi na mashirika ya Kimataifa kama UNESCO na UNICEF.
“Kwa hiyo, hayo yote tumekuwa tukishirikiana nayo ili kufikisha dhamira nzima ya Serikali kwamba TEHAMA inatumika na inaleta mapinduzi ya kiuchumi kwa ujumla.
"Tunapozungumzia uchumi wa kidijitali na mabadiliko ya teknolojia yanaleta taswira tofauti ya mfumo wa ajira baada ya miaka mitano au 10 ijayo.
"Kwa mfano leo hii tunaona kuna makampuni ya Kimataifa kama alivyosema mwenzangu kuna Ubber, kuna Bolt, kuna Airbnb wanasema Dunia nzima ameweza kuajiri watu 7,300.
"Na kuna watu hapa Tanzania wanafanya Airbnb, lakini hajui waliko, Airbnb ni kampuni ya Kimarekani."
Amesema, hiyo inaleta picha kwamba kama nchi hatuna namna ya kukimbia hayo mabadiliko. “Ni lazima tutengeneze nguvu kazi ambayo itahisi hayo mabadiliko ya kiuchumi kwa miaka mitano au 10 inayokuja.”
Mhandisi Zuberi anabainisha kuwa, kwa mazingira hayo unajikuta hasa ukija hapa nchini kuna changamoto ya elimu ambapo unakuta wapo vijana.
“Sisi tunapotengeneza bunifu, mfano tuseme kuangazia changamoto zilizopo Tanzania, ukija kwetu unakuta sehemu ya vijana hawana ufikiwaji wa elimu au maarifa ya kutosha kuweza kuwawezesha kutengeneza bunifu zao ambazo zinahakisi mazingira halisi ya kiuchumi.
“Kwa hiyo, maana hapa mwenzetu wa Tume ya TEHAMA anazungumzia uhitaji wa ujenzi wa vituo vya ubunifu wa nchi nzima, lakini pia kuna changamoto ya mitaji.”
Amesema, wamekuwa wakikutana na vijana wenye bunifu nzuri, lakini changamoto inakuwa ni mtaji pale ambapo anataka kupanua ubunifu wake.
“Kwa hiyo, unajikuta sisi kama Serikali kupitia wizara yetu, tuna shughuli tunaendelea nayo ya uboeshaji wa sera zilizopo au kuanzisha sera mpya ambayo itazungumzia namna gani kampuni changa hizi startups zinaweza zikajiendesha vizuri nchini, kwa kuweka hayo mazingira.
“Kwa hiyo, pengine sera itatoa muongozo ni namna gani watapata mitaji kwa urahisi, masuala ya kufaidika kwenye kodi ambazo hizo ndiyo changamoto, elimu juu ya namna gani wataweza kukuza bunifu ili waweze kushindana duniani kwa ujumla.”
Amesema, changamoto kubwa ni kukosa mitaji, maarifa ya kutosha ili kuweza kushindana duniani na namna ya kuyapata masoko.
“Tunaona, mfano NALA, huyu amepata jukwaa nzuri na amejulikana kImataifa, lakini haimaanishi kwamba hatuna bunifu nyingine ambazo ni nzuri na zinaweza zikafanya vizuri duniani, kwa hiyo sisi kama Serikali tunaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha wale ambao wanafanya vizuri, basi tunawauza Kimataifa, lakini kuongea na kampuni binafsi, benki ili kuhakikisha wanapata mitaji.”
Pia, amesema wataangalia namna ya kupunguza kodi na namna ya kupata leseni za biashara kwa gharama nafuu ukilinganisha na mfanyabiashara ambaye amekuwa vizuri.
Usawa kwenye bunifu
“Suala la usawa wa kijinsia kwenye bunifu lipo, na ndiyo maana linazungumzwa Dunia nzima, lakini tayari sisi tumeanzisha program nyinginyingi tu, kwa mfano mwezi huu tulikuwa tunaadhimisha duniani Siku ya TEHAMA kwa Wanawake.”
Amesema, kupitia siku kama hiyo watoto wa kike huwa wanapewa fursa ya kushindana na kuonesha uzoefu au ubunifu walionao katika TEHAMA.
“Lakini, tunapozungumzia kwa mfano ujenzi wa maabara kwenye mashule, hatulengi kugusa kundi moja wapo, ni kwamba tunaamini hata kupitia zile maabara za TEHAMA basi watoto wa kike wataweza kunufaika.
“Kwa hiyo, tunaendelea kuwahamasisha na ninadhani mfano mmoja wapo ukizungumzia masuala ya TEHAMA, utatukuta wanawake tupo juu.”