WASHINGTON-Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya nchi kupitia misaada, mikopo nafuu na utaalamu wa kiufundi ambao Taasisi hiyo kubwa ya Fedha Dunia inaipatia Tanzzania kwa miongo kadhaa sasa.

Pamoja na kuishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha zinazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, Dkt. Nchemba alionesha furaha yake kwa Benki ya Dunia kuonesha utayari wake wa kusaidia ujenzi wa mradi mkubwa wa kimkakati wa Reli ya Kisasa (SGR).
Aidha, Mhe. Dkt. Nchemba alimkumbusha Dkt. Kibwe, kuhusu maombi ya Tanzania ya kutaka Kiswahili kiwe sehemu ya lugha rasmi za mawasiliano katika mikutano ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia kutokana na umuhimu wake katika maendeleo ya Bara la Afrika na Dunia kwa ujumla.
Katika kikao hicho pia alishiriki Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo, aliyezungumzia kuhusu kuanza kwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 itakayosaidia kuchochea maendeleo ya watu na kukuza uchumi wa nchi, huku Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, aliyeshukuru kwa mchango wa Benki ya Dunia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Zanzibar.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, anayesimamia Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency), ambaye ni Mtanzania, Dkt. Zarau Wendeline Kibwe, alisema Benki ya Dunia inathamini ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Benki yake na Tanzania.


Tags
Benki ya Dunia (WB)
Dr Mwigulu Lameck Nchemba
Habari
International Monetary Fund (IMF)
Kimataifa
Wizara ya Fedha Tanzania