Waziri Kombo awasili nchini Angola

LUANDA-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amewasili jijini Luanda, Angola ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Angola inayotarajiwa kufanyika tarehe 7 hadi 9 Aprili, 2025.
Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa 4 de Fevereiro, Waziri Kombo alipokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola anayeshughulikia Masuala ya Utawala na Fedha, Mhe. Balozi Osvaldo dos Santos Varela, Balozi wa Angola nchini Tanzania, Mhe. Sandro de Oliveira na Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lut. Jen Edward Mkingule, ambaye pia anaiwakilisha Tanzania nchini Angola.
Katika ziara hiyo, Mhe. Kombo ameambatana na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Shaaban Ali Othman, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, pamoja na maafisa Wengine wa Serikali kutoka wizara na taasisi mbalimbali za umma.

Mhe. Waziri Kombo anatarajiwa kushiriki katika vikao vya maandalizi na mazungumzo ya awali na ujumbe wa Tanzania uliooko nchini humo kwa lengo la kuweka msingi madhubuti wa ziara hiyo ya kihistoria ya Mhe. Rais Samia.
Ziara hiyo ni ya kihistoria, kwani ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa Tanzania kutembelea Angola katika kipindi cha miaka 19. Mara ya mwisho kwa kiongozi wa juu kufanya ziara nchini humo ilikuwa mwaka 2006, wakati Rais Mstaafu, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipotembelea Angola.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news