DODOMA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Wizara yake imepanga kutekeleza vipaumbele 14 katika mpango wa bajeti wa mwaka 2025/26.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara na taasisi zake kwa mwaka 2025/26, Mhe. Mchengerwa amesema utekelezaji wa mpango wa majeti unazingatia vipaumbele vya kusimamia shughuli za utawala bora, kukuza demokrasia, ushirikishwaji wa wananchi na Ugatuaji wa Madaraka kwa Umma (D by D).
Pia kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za utoaji wa huduma za jamii, kuratibu na kusimamia mkakati wa kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi yasiyo na tija katika ngazi zote na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
Mchengerwa amesema kufanya uratibu wa usimamizi wa mifumo ya TEHAMA, kuendeleza rasilimali watu katika ngazi zote za Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kuratibu na kusimamia shughuli za kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, mikoa na mamlaka za serikali za mitaa na kuratibu na kushiriki michezo ya shule za msingi (UMITASHUMTA), sekondari (UMISSETA) na mashindano ya michezo ya shule za sekondari za Afrika Mashariki.Amesema,pia kuratibu shughuli za utendaji wa kazi wa taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, kuratibu na kusimamia ujenzi wa miradi ya maendeleo katika ngazi zote za Ofisi ya Rais-TAMISEMI, kuratibu uibuaji wa miradi ya kimkakati na miradi inayopaswa kutekelezwa kwa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika mamlaka za serikali za mitaa na kusimamia na kuratibu shughuli za utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa maliasili katika mikoa na mamlaka za serikali za mitaa.
Kipaumbele kingine ni kuratibu na kusimamia utekelezaji wa afua za mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa utalii, uhamasishaji wa nishati.Shilingi trilioni 11.8
Awali, Waziri Mchengerwa amewasilisha bungeni makadirio ya mapato kwa mwaka 2025/26 yenye takribani Shilingi trilioni 11. 783 kwa ajili ya wizara na taasisi zilizo chini yake.
Bajeti hiyo imeongezeka kutoka Shilingi trilioni 10.125 zilizotengwa mwaka 2024/25 hadi kufikia Shilingi trilioni 11.783 na kuwa na ongezeko la zaidi ya Sh trilioni 1.66.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amesema Shilingi trilioni 3.95 zinaombwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo kati ya fedha hizo Shilingi trilioni 2.5 ni fedha za ndani, ikijumuisha Shilingi bilioni 613.44 za mapato ya ndani ya halmashauri na Shilingi trilioni 1.45 ni fedha za nje.
Pia amesema Shilingi trilioni 7.84 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida yanayojumuisha mishahara Shilingi trilioni 6.3 na matumizi mengineyo Shilingi trilioni 1.53 ikijumuisha Shilingi trilioni 1. 067 za mapato ya ndani ya halmashauri.
“Tumewasilisha si tu makadirio ya mapato na matumizi, bali tumeweka mbele yetu dira ya matumaini, ramani ya maendeleo na ahadi ya uongozi unaowajibika. TAMISEMI haitafuti sifa ya kisiasa, tunatafuta suluhisho sahihi kwa maisha ya mtanzania wa kawaida.”
Aidha, Mchengerwa ametoa wito kwa mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na wananchi wote kushirikiana, kusonga mbele kwa mshikamano.
“Kwa dhamira hii, na kwa imani kubwa katika maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunawasilisha bajeti hii kama zana ya kazi, dira ya matumaini na silaha ya mapinduzi ya kiutawala, kiuchumi na kijamii.”
“Kwa dhamira hii, na kwa imani kubwa katika maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunawasilisha bajeti hii kama zana ya kazi, dira ya matumaini na silaha ya mapinduzi ya kiutawala, kiuchumi na kijamii.”“Kwa hiyo, tunasema kwa ujasiri mkubwa, TAMISEMI, ndiyo msingi wa maendeleo endelevu. Kila Shilingi ina Jukumu, Kila Kiongozi ana Wajibu na Kila Mwananchi ana Nafasi!”
